Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mabaharia, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Juni, Katibu Mkuu amesema karibu asilimia 90 ya bidhaa na mahitaji muhimu duniani, ikiwemo chakula, dawa na nishati, husafirishwa kwa njia ya bahari.

“Ni meli na mabaharia wanaoufanya ulimwengu kuendelea kusonga mbele,” amesema.

Katibu Mkuu ameeleza kuwa migogoro na mivutano ya kisiasa inaendelea kuwaweka mabaharia katika hatari, akitaja matukio ya hivi karibuni katika Mlango wa Hormuz yaliyowaacha makumi ya maelfu ya mabaharia wakiwa wamekwama huku wakifanya kazi mbali na familia zao.

“Matukio ya hivi karibuni katika Mlango wa Hormuz yamewaacha makumi ya maelfu ya mabaharia wakiwa wamekwama huku wakifanya kazi mbali na nyumbani ili kuhakikisha dunia inaendelea kupata mafuta na chakula,” amesema.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Mabaharia, “Kubeba biashara ya dunia. Kubeba hatari zake.”, inaangazia changamoto na hatari zinazowakabili wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa baharini wanapowezesha biashara ya kimataifa kuendelea.

Katibu Mkuu amesisitiza, “mabaharia kamwe hawapaswi kuwa wahanga au kutumiwa kama nyenzo katika migogoro ya kijiografia.”

Amezitaka serikali na sekta ya usafirishaji wa baharini kutimiza wajibu wao wa kuwalinda mabaharia kwa kuheshimu viwango vya kazi, sheria za kimataifa na kuhakikisha usalama wao mahali pa kazi.

Aidha, amesema watu wengi wasiokuwa karibu na bahari mara nyingi hawatambui umuhimu wa usafiri wa baharini hadi pale kunapotokea mgogoro au usumbufu katika usafirishaji.

Katika maadhimisho ya siku hii, Katibu Mkuu ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutambua mchango, ujasiri na ustahimilivu wa mabaharia duniani.

“Tuwaheshimu mabaharia kwa ujasiri na ujuzi wao, na tusimame pamoja nao katika kukabiliana na dhoruba zote,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *