Dar es Salaam. Shughuli za usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz zimeanza kurejea taratibu baada ya Umoja wa Mataifa kuzindua mpango maalumu wa kuondoa mamia ya meli zilizokwama katika eneo la Ghuba kufuatia miezi kadhaa ya vita na mvutano wa kijeshi kati ya Iran, Marekani na Israel.

Kwa mujibu wa Deutsche Welle (DW), meli zilianza tena kupita katika njia hiyo muhimu jana Jumatano Juni 24, 2026 chini ya usimamizi wa Shirika la Kimataifa la Baharini (IMO), ambalo ni wakala wa Umoja wa Mataifa unaosimamia usalama wa usafiri wa baharini duniani.

Hormuz ni njia nyembamba inayounganisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman. Njia hiyo hubeba sehemu kubwa ya mafuta na gesi inayouzwa katika masoko ya dunia, hivyo kufungwa kwake kulisababisha wasiwasi mkubwa katika sekta ya nishati na biashara ya kimataifa.

Mzozo huo ulioanza Februari 28, 2026 baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran, ulisababisha vita vilivyodumu kwa takribani miezi minne.

Wakati wa mapigano hayo, Iran ilidhibiti eneo la Hormuz na usafirishaji wa mafuta na gesi ulivurugika kwa kiwango kikubwa.

Kwa mujibu wa Reuters, Juni 11 makamanda wa kijeshi wa Iran walitangaza kufungwa kwa Hormuz kufuatia mashambulizi ya Marekani, wakionya kuwa meli yoyote ambayo ingepita bila ruhusa ingeshambuliwa.

Hatua hiyo ilisababisha mamia ya meli na zaidi ya mabaharia 11,000 kubaki wamekwama katika eneo la Ghuba huku kampuni nyingi za usafirishaji zikisitisha safari zake.

Mabadiliko yalianza kuonekana wiki iliyopita baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, na viongozi wa Iran kufikia makubaliano ya awali ya kusitisha vita.

Makubaliano hayo yalifungua njia ya mazungumzo ya siku 60 kuhusu masuala yaliyosalia, ikiwemo mpango wa nyuklia wa Iran na usalama wa usafiri katika Hormuz.

Katibu Mkuu wa IMO, Arsenio Dominguez amesema operesheni ya sasa ya kupitisha meli ni matokeo ya mazungumzo yaliyohusisha Iran, Oman, Marekani, mataifa mengine ya mwambao wa Ghuba pamoja na sekta ya usafiri wa baharini.

“Kazi hii kubwa inafanyika kwa ushirikiano wa karibu na Iran, Oman, mataifa yote ya mwambao wa eneo husika, Marekani na wadau wa sekta ya baharini,” Reuters imemnukuu Dominguez akisema.

Mpango huo unahusisha utaratibu maalum ambapo kila meli inapangiwa muda wake wa kupita ili kupunguza hatari za msongamano, migongano au kukutana na mabomu ya baharini yanayodaiwa kuwepo katika baadhi ya maeneo ya njia hiyo.

Hata hivyo, hali bado si shwari. DW imeripoti kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) limetangaza kuwa meli zitapaswa kutumia njia zilizoidhinishwa na Tehran pekee.

Jeshi hilo limesema njia mpya zilizotangazwa bila uratibu na Iran hazikubaliki na linaweza kuchukua hatua dhidi ya meli zitakazokiuka masharti hayo.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio ameanza ziara katika nchi za Ghuba kutafuta uungwaji mkono wa washirika wa Marekani kuhusu makubaliano mapya na Iran.

Tayari, Rubio ameshakutana na viongozi kadhaa Abu Dhabi, wakiwemo Rais wa Falme za Kiarabu, Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, pamoja na mshauri wa usalama wa taifa, Sheikh Tahnoun bin Zayed Al Nahyan na Waziri wa Mambo ya Nje, Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, viongozi hao wamejadili makubaliano ya muda kati ya Washington na Tehran pamoja na usalama wa usafiri katika Hormuz.

Rubio amewahakikishia washirika wa Marekani kuwa nchi yake haitafanya jambo lolote litakalohatarisha usalama wao.

Licha ya kurejea kwa shughuli za usafirishaji, wataalamu wa sekta ya meli wanaonya kuwa hali ya kawaida bado haijafikiwa.

Kwa sasa, Hormuz imefunguliwa lakini chini ya uangalizi mkali wa Umoja wa Mataifa na kwa tahadhari kubwa kutoka kwa pande zote.

Hatua hiyo imeanza kurejesha matumaini katika biashara ya kimataifa, ingawa mustakabali wa usalama wa njia hiyo bado utategemea mafanikio ya mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran, Marekani na mataifa ya Ghuba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *