
Mwenge ni mwanzilishi na mratibu wa shirika la Action Intervention des Femmes Entrepreneurs pour le Développement, linalojikita katika kulinda na kuwawezesha wasichana walio chini ya umri wa miaka 18, hususan wale manusura wa ubakaji, kupoteza familia zao au kulazimika kuishi mitaani.
“Tunawaelimisha wasichana kuhusu haki zao, tunawasaidia waliobakwa, na tunafanya kazi na familia na mamlaka kuhakikisha wanapata haki na ulinzi wanaostahili,” anasema Mwenge.
Kwa mujibu wake, wengi wa wasichana hao walipoteza wazazi wakati wa mashambulizi ya makundi yenye silaha, huku wengine wakilazimika kukimbia makazi yao na kuishia mitaani ambako hukumbana na unyanyasaji zaidi.
Vita vinapopora ndoto za utoto
Kila siku, Mwenge na timu yake hukutana na simulizi za kutisha za watoto waliopitia mateso makubwa kuliko umri wao.
Baadhi ya wasichana wanaowasaidia walibakwa wakati wakikimbia mapigano, wengine walishuhudia wazazi wao wakiuawa mbele yao, huku wengine wakibaki bila mtu wa kuwahudumia.
“Tunawapokea watoto hawa, tunawapeleka kupata matibabu, ushauri nasaha na tunafanya kazi na serikali kuhakikisha wanapata haki zao,” anasema.
Kwa wale waliopata maambukizi ya virusi vya UKIMWI au VVU kutokana na ukatili wa kingono, shirika hilo huwasaidia kupata dawa na msaada wa kisaikolojia ili waweze kuendelea na maisha.
Lakini changamoto kubwa zaidi, Lydie anasema, ni kwamba vita havikomi.
“Unamwokoa msichana, unamfundisha kazi ya kujitegemea, unaanza kuona matumaini. Kisha vita vinarudi tena. Analazimika kukimbia, anakutana tena na wale waliomdhuru, na safari inaanza upya kutoka sifuri.”
Kauli hiyo inaonesha jinsi mzunguko wa vurugu unavyofuta mafanikio ya miezi au hata miaka ya kazi ya kuwasaidia manusura.
Kurejesha familia, kurejesha matumaini
Moja ya kazi zinazogusa zaidi moyo kwa shirika hilo ni kuunganisha watoto waliopotea na familia zao.
Mwenge anakumbuka visa vya watoto waliotenganishwa na wazazi wao wakati wa mapigano na kukaa kwa muda mrefu bila kujua walipo ndugu zao.
“Tukimpata mtoto aliyepoteza familia yake, tunaanza kutafuta ndugu zake. Tukiwapata, tunawaunganisha tena. Huo ni ushindi mkubwa kwetu.”
Kwa watoto ambao familia zao haziwezi kupatikana, shirika hutafuta familia mbadala zinazoweza kuwalea na kuwapa mazingira salama ya kukulia.
“Mahali pa mtoto ni ndani ya familia, si barabarani,” anasisitiza.
Anasema ni jambo la kuhuzunisha kuona wasichana wenye umri wa miaka 13 au 14 wakitumiwa kingono na wanaume wengi ili kupata chakula au mahali pa kulala.
“Furaha yetu ni kumwona msichana akitoka mitaani, anarudi shule au anaanza kazi ya kujitegemea, na polepole anasahau maumivu aliyopitia.”
Ushirikiano na Umoja wa Mataifa
Katika kazi yake, Mwenge anashirikiana na mamlaka za serikali pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo Shirila na masuala ya wanawake UN Women na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani nchini humo MONUSCO na mashirika yanayolenga kulinda wanawake na watoto.
Anasema msaada wa Umoja wa Mataifa katika kufuatilia matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu umekuwa muhimu katika kuhakikisha waathirika wanatambuliwa na kupata msaada.
“Ufuatiliaji huo unatupa uwezo wa kujua kilichotokea, nani alihusika na jinsi ya kusaidia manusura wa ubakaji kupata haki.”
“Tunachohitaji zaidi ni amani”
Licha ya mafanikio yaliyopatikana, Mwenge anaamini suluhisho la kudumu kwa mateso ya watoto wa mashariki mwa DRC ni kumalizika kwa vita.
“Kitu bora tunachotafuta ni vita viishe. Vita vikikoma, watoto watapata haki zao, watarudi kwa familia zao na wataweza kuishi maisha ya kawaida.”
Anatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono juhudi za amani na ulinzi wa watoto nchini DRC.
Lydie amesisitiza kuwa “Watoto hawa hawakuchagua kuzaliwa katikati ya vita. Wanastahili nafasi ya kusoma, kucheza na kuota ndoto kama watoto wengine duniani.”
Kwa Mwenge, kila msichana anayerejea shule, kila mtoto anayepata familia na kila manusura anayepata sababu ya kutabasamu tena ni ushahidi kwamba hata katikati ya vita, matumaini bado yanaweza kushinda.