Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kwamba hakuna hospitali yoyote katika Ukanda wa Gaza inayofanya kazi kwa uwezo wake kamili kwa sasa, na kwamba, uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu na mafuta umeweka utoaji wa huduma za afya katika hatari kubwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Quds (Qudsna), likinukuu Shirika la Habari la Shafaq, shirika hilo lilionya kuwa uhaba unaoendelea wa mafuta na vifaa vya matibabu umeongeza hatari ya kusitishwa kwa mamia ya upasuaji na huduma muhimu za matibabu katika vituo vya afya vya Gaza.

Shirika la Afya Duniani pia limesisitiza kuwa mfumo wa afya wa Gaza uko chini ya shinikizo kubwa na kwamba vituo vya afya vinakabiliwa na vikwazo vikubwa katika kukidhi mahitaji yao ya msingi.

Aidha hivi karibuni Shirika la Afya Dunia (WHO) lilitahadharisha kuhusu hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa, watoto zaidi ya 8,000 wenye chini ya miaka 5 huko Gaza wanasumbuliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu kutokana na vita vya kikatili na vya mauaji ya kimbari ya utawala haramu wa Israel.

Hayo yanajiri katika hali ambayo mashirika mbalimbali ya kieneo na kimataifa yameendelea kutahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Mfuko wa Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa (UNPF) umetahadharisha kuhusu taathira hasi za utapiamlo zinazowakodolea macho wanawake wajawazito na watoto wachanga katika Ukanda wa Gaza; huku vita vya kikatili na vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo hilo vikishadidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *