“Taratibu za uteuzi na uajiri wa majaji, ambazo ni lango la kuingia katika mifumo ya mahakama, lazima ziundwe kwa namna inayolinda uhuru na kutopendelea kwa mhimili wa mahakama tangu mwanzo,” amesema Margaret Satterthwaite, Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhuru wa Majaji na Wanasheria.

Akiwasilisha ripoti yake kwa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, Satterthwaite amesema mifumo ya uteuzi wa majaji lazima ihakikishe wanaochaguliwa wana uwezo, maadili na uadilifu wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi hata wakati wa migogoro au shinikizo.

“Taratibu za uteuzi zinapaswa kuhakikisha wanaoteuliwa kuwa majaji wana uwezo na hulka ya kutumikia kwa weledi na maadili, hata wakati wa misukosuko,” amesema.

Katika ripoti yake, ameeleza misingi muhimu ya kulinda mchakato wa uteuzi wa majaji dhidi ya ushawishi usiofaa kutoka kwa wanasiasa, wenye nguvu kiuchumi au hata makundi ya uhalifu wa kupangwa.

Misingi hiyo ni pamoja na:
• Kuwepo kwa mifumo ya kisheria iliyo wazi kuhusu uteuzi wa majaji
• Vyombo huru na visivyoegemea upande wowote kusimamia mchakato wa uteuzi
• Kutumia vigezo vya wazi vinavyolenga sifa, uwezo na uadilifu
• Kuhakikisha utofauti na uwakilishi katika mhimili wa mahakama
• Kuwepo kwa fursa ya ushiriki wa asasi za kiraia na wadau wengine

Satterthwaite amezitaka nchi wanachama kuweka mipaka madhubuti kwa uteuzi wa muda au wa mpito wa majaji, akionya kuwa hali hiyo inaweza kuongeza uwezekano wa ushawishi usiofaa.

“Uwazi ni msingi katika kila hatua ya mchakato. Ni muhimu pia kuweka mifumo madhubuti ya kupinga kasoro katika uteuzi na kuhakikisha ushiriki wa maana wa asasi za kiraia,” amesema.

Margaret Satterthwaite ni Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhuru wa Majaji na Wanasheria, yeye ni mmoja wa wataalamu huru wanaoteuliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *