
Kupitia taarifa iliyotolewa leo Juni 26 jijini Kinshasa, WFP imeonya kuwa bila msaada wa haraka, kuongezeka kwa njaa, ukosefu wa usalama na kuhama kwa watu kunaweza kufanya iwe vigumu kwa familia kufuata hatua za kiafya zinazopendekezwa, jambo ambalo linaweza kuongeza hatari ya maambukizi zaidi.
Hali ya afya na uhakika wa chakula mashariki mwa DRC
Maambukizi ya Ebola yanaendelea kuripotiwa katika Jimbo la Ituri na kaskazini mwa Kivu Kaskazini, hali inayohitaji hatua endelevu za kudhibiti ugonjwa huo ili kuzuia kuenea zaidi ndani na nje ya maeneo yaliyoathirika.
Virusi hivyo sasa vimeathiri kanda 34 za afya katika Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini. Kati ya maeneo hayo, 30 tayari yanakabiliwa na viwango vya juu vya njaa (IPC Awamu ya 3 au zaidi), huku maeneo saba yakikumbwa na kiwango cha dharura cha njaa (IPC Awamu ya 4).
Zaidi ya watu milioni 10 katika mashariki mwa DRC wanakabiliwa na ukosefu wa chakula, hali inayozifanya familia nyingi kushindwa kukabiliana na mshtuko mwingine wa kibinadamu.
Msaada wa chakula kutoka WFP
WFP kwa sasa inasaidia zaidi ya watu milioni 1.2 kupitia msaada wa chakula, lishe, usafirishaji, mawasiliano na huduma za ndege zinazosaidia kuendeleza mwitikio wa sekta ya afya.
Tangu Mei 28, zaidi ya milo moto 36,000 imetolewa kwa wagonjwa, walezi na watu waliokaribiana na wagonjwa katika vituo 14 vya matibabu na karantini.
Zaidi ya watu 2,600 katika Kivu Kaskazini na Ituri wamepokea mgao wa chakula wa kubeba nyumbani, huku watu 14,000 katika vijiji kumi vilivyowekwa karantini Kivu Kusini wakipata msaada wa chakula wa kila mwezi.
Shirika hilo pia linaendesha shughuli za lishe katika maeneo saba ya afya yaliyoathirika. Hata hivyo, changamoto katika uchunguzi wa lishe na mifumo dhaifu ya kuainisha wagonjwa zinaendelea kuzuia utoaji wa huduma zinazolengwa.
Mkanganyiko wa Ebola, vita na njaa – Kisa cha Jack
Ebola ikiendelea kusambaa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), katikati ya moja ya janga kubwa zaidi la njaa duniani, mapigano yanayoendelea yanawalazimisha watu kuhamia katika maeneo ya afya yaliyokumbwa na ugonjwa huo ambao aina yake ya sasa ambayo ni Bundibugyo haina tiba wala chanjo.
Mwakilishi Mkazi wa WFP nchini humo David Stevenson kupitia ukurasa wa X zamani Twitter ametumia mfano kuelezea changamoto zitokanazo na mkanganyiko huo wa ugonjwa, njaa na mapigano.
“Ningependa kutoa mfano mmoja tu. Hivi karibuni, timu yetu ilikutana na Jack, baba aliyekimbia makazi yake kutokana na mapigano. Binti yake mwenye umri wa miaka mitano alifariki kwa Ebola. Alikimbia mapigano huko Bukavu jimboni Kivu Kusini na kutembea kwa siku kadhaa hadi Beni jimboni Kivu Kaskazini, akidhani ameepuka hali mbaya zaidi,” amesema Mkuu huyo wa WFP nchini DRC.
“Lakini binti yake alianza kuugua homa kali na kutokwa damu masikioni. Alimkimbiza hospitalini, lakini hakufanikiwa kuokoa maisha yake. Wiki mbili baadaye, mke wake bado yuko katika kituo cha kutengwa kwa ajili ya uangalizi,” amesema Bwana Stevenson.
Ili kuhakikisha wagonjwa na waambata wao wanasalia kwenye vituo vya karantini, WFP inatoa milo ya moto ili wagonjwa na waliokutana nao wasilazimike kutoka kutafuta chakula.
Jack mwenyewe sasa anawatunza wanafamilia 13 kwa msaada wa chakula kutoka WFP ingawa hivyo aliwauliza WFP swali rahisi lakini chungu. “Kwa watoto wote hawa, mgao huu wa chakula wa mwezi mmoja utadumu kwa wiki mbili tu. Baada ya hapo, nitawalishaje ilhali sina njia yoyote ya kufanya hivyo?”
Milo ya moto ziliko familia na wagonjwa ni jawabu
Tangu mlipuko huu uanze, WFP imesambaza zaidi ya milo ya moto 36,000 katika vituo vya matibabu ya Ebola, mgao wa chakula wa kubeba nyumbani kwa watu 2,600 jimboni Kivu Kaskazini na Ituri, pamoja na chakula cha kila mwezi kwa watu 14,000 katika vijiji 10 vilivyo chini ya karantini huko jimboni Kivu Kusini ambavyo vimeathiriwa vibaya na mlipuko wa Ebola.
“Lakini tunahitaji kufanya zaidi,” amesema Afisa huyo wa WFP akiongeza kuwa, “ na tunahitaji kufanya hivyo kwa haraka, kwa kiwango kikubwa na kwa rasilimali zinazohitajika. Kwa familia kama ya Jack, hili ni jambo halisi. Tukichukua hatua sasa kwa haraka, tutakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kudhibiti Ebola na kuzuia mgogoro huu mkubwa wa kibinadamu usizidi kuwa mbaya.”
Usafirishaji na usambazaji wa misaada
WFP inaendelea kuwa mhimili mkuu wa usafirishaji katika mwitikio wa Ebola, ikisaidia washirika wa afya na misaada kuwafikia wananchi walioathirika kwa haraka na kwa usalama.
Huduma ya Umoja wa Mataifa ya Msaada wa Kibinadamu kwa njia ya ndege (UNHAS) inayosimamiwa na WFP imefanya safari 268 za ndege, kusafirisha zaidi ya wahudumu 1,750 wa kibinadamu na kupeleka tani 36 za mizigo muhimu katika maeneo ya mstari wa mbele.
UNHAS inaendesha safari za kila siku zinazounganisha Kinshasa, Bunia, Beni na maeneo mengine yenye kipaumbele katika kukabiliana na mlipuko huo.
Ndege zilizokodishwa na WFP pia zimesafirisha karibu tani 154 za vifaa vya matibabu, vifaa vya kujikinga, vifaa vya maabara na mizigo mingine ya kuokoa maisha katika maeneo yaliyoathiriwa na Ebola.
Helikopta maalum imewekwa kusaidia kufikia maeneo yenye maambukizi makubwa kama Mongbwalu na Nyakunde.
Aidha, ndege ya Hercules C-130 imesafirisha mizigo muhimu kutoka Uganda hadi Bunia, ambapo zaidi ya tani 150 za vifaa muhimu tayari zimewasilishwa.
Vitengo vitatu vya kutenga wagonjwa vya Epishuttle pia vimewekwa Bunia ili kusaidia kuhamisha kwa usalama wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola, huku mafunzo ya usafiri wa wagonjwa wa dharura yakifanyika kwa kushirikiana na wadau wengine.
WFP na washirika wake wanaendelea kupanua huduma katika maeneo mapya yaliyoathirika yakiwemo Butembo, Bambu, Kilo, Nizi, Tchomia na Kasenyi, ambako njaa kali na watu kuhama makazi yao tayari ni tatizo kubwa.
Changamoto na mahitaji ya fedha
Ukosefu wa usalama na ugumu wa kufikia baadhi ya maeneo unaendelea kuwa kikwazo kikubwa, kwani maeneo mengi yaliyoathirika yako karibu na maeneo ya mapigano na jamii nyingi zinalazimika kuhama kutafuta chakula na usalama.
WFP inahitaji kwa dharura dola milioni 72 za Marekani katika kipindi cha miezi sita ijayo ili kuendelea na msaada wa chakula, huduma za UNHAS na shughuli za usafirishaji zinazohusiana na mwitikio wa Ebola.
Kwa ujumla nchini DRC, shirika hilo linahitaji dola milioni 286 katika miezi sita ijayo ili kuendelea kutoa msaada muhimu wa chakula.
WFP imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu watu walio katika mazingira magumu waliokwama katika maeneo yasiyofikika, ambapo njaa na utapiamlo vinaweza kuongezeka kadri msimu wa uhaba wa chakula unavyokaribia.