
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuimarisha juhudi za kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya na biashara haramu ya dawa hizo, akionya kuwa tatizo hilo linaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na jamii duniani kote.
Katika ujumbe wake wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi Mabaya ya Dawa za Kulevya na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Juni ikilenga kuongeza uelewa kuhusu athari za dawa za kulevya kwa afya, jamii na maendeleo, Guterres amesema biashara haramu ya dawa za kulevya si uhalifu usio na waathirika, bali ni tatizo linalochochea vurugu, uhalifu na kuyumbisha utulivu wa jamii.
“mesema. “Tunapoadhimisha siku hii ya kimataifa, na tujitolee upya katika kutekeleza suluhisho thabiti, za kibunifu na zinazotegemea ushahidi ambazo janga hili linahitaji,”
Katibu Mkuu amesema changamoto hiyo inaendelea kuwa kubwa zaidi kutokana na kuongezeka kwa dawa za kulevya zinazotengenezwa viwandani pamoja na kukua kwa mitandao ya biashara haramu kupitia mtandao wa intaneti.
Ameeleza kuwa mifumo dhaifu ya afya, mapungufu katika huduma za matibabu na ukosefu wa huduma za msaada vinaendelea kudhoofisha juhudi za kusaidia waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza umuhimu wa kutumia ubunifu, teknolojia na ushirikiano katika kukabiliana na tatizo hilo linalozidi kuathiri afya ya umma na usalama wa jamii.
Guterres amesema matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya mtandaoni, huku akitaka ushirikiano zaidi kati ya vyombo vya sheria na mamlaka husika ili kuvunja mitandao ya kihalifu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika kinga, kupunguza madhara na matibabu, akisema hatua hizo ni muhimu katika kujenga jamii salama na zenye afya bora.