Maelfu ya wananchi wa Lebanon wamejitokeza mitaani katika miji na maeneo mbalimbali kupinga “makubaliano” yanayoungwa mkono na Marekani kati ya Lebanon na utawala wa Israel, huku wakiyataja kuwa tishio kwa mamlaka ya taifa lao.

Usiku wa Ijumaa, maandamano yalisambaa katika mji mkuu Beirut na maeneo mengine ya Lebanon baada ya serikali kutangaza kuwepo kwa makubaliano hayo yanayoungwa mkono na Marekani na yanayohusisha utawala wa Israel.

Waandamanaji walikusanyika katika eneo la Ramlet al-Bayda, karibu na makao ya serikali, pamoja na katika vitongoji kadhaa vya mji mkuu, wakionyesha hasira yao kuhusu makubaliano hayo na kukataa hatua yoyote ya kuelekea mazungumzo ya moja kwa moja na dola ya kikaliaji.

Waandamanaji walifunga barabara kuu katika eneo la Salim Salam na kuchoma matairi, huku maandamano yanayofanana na hayo yakiripotiwa pia katika Msharafiyeh na maeneo ya kusini mwa Beirut.

Mijumuiko ya amani pia imepangwa katika maeneo kadhaa, ambapo washiriki walitaka makubaliano hayo yafutwe na kuonya dhidi ya aina yoyote ya ushirikiano wa kisiasa au wa kidiplomasia na Israel.

Maandamano hayo yalifuatia tangazo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, aliyesema kuwa makubaliano yalikuwa yamefikiwa kati ya Lebanon na Israel.

Balozi wa Israel mjini Washington, Yechiel Leiter, alikaribisha hatua hiyo, akidai kuwa chini ya mfumo huo, “Hizbullah imeondolewa nje ya mahesabu.”

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, pia ameyasifu makubaliano hayo na kuyataja kuwa mafanikio makubwa kwa utawala huo.

Mufti Mkuu wa Madhab ya Ja’afari nchini Lebanon, Sheikh Ahmad Qabalan, amekosoa vikali makubaliano hayo yanayoungwa mkono na Marekani kati ya serikali ya Beirut na utawala wa Tel Aviv, akisema kwamba makubaliano hayo hayana uhalali.

Ameongeza kuwa: “Jambo la hatari ni kwamba mfumo huu wa makubaliano unalipa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel mamlaka ya kiutendaji katika shughuli za jeshi la Lebanon na pia juu ya maeneo ya Lebanon yaliyo chini ya uvamizi.”

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kishia wa Lebanon amebainisha kuwa makubaliano hayo yanamaanisha kukubali kimyakimya utawala wa kijeshi wa Israel juu ya maeneo ya Lebanon yaliyochukuliwa kwa nguvu.

Tangu Machi 2, wakati Israel ilipoanzisha mashambulizi yake ya hivi karibuni dhidi ya Lebanon, vikosi vya utawala huo vimeua angalau watu 3,600 na kujeruhi wengine 11,000 nchini humo.

Katika kkujibu mashambulizi hayo, harakati ya Hizbullah, imeendelea na operesheni za kijeshi dhidi ya vikosi vya Israel katika eneo la mpaka.

Hati ya Makubaliano ya Maelewano ya Islamabad (MoU) iliyotiwa saini na Iran na Marekani mwezi Juni inajumuisha vipengele vinavyotaka kusitishwa kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon pamoja na kuheshimiwa kwa mamlaka ya taifa hilo na ukamilifu wa ardhi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *