TIMU mbili za Kilimanjaro Wonders na Bunda Girls ya Mara zimepanda Ligi Kuu ya Wanawake msimu ujao, baada ya kufanya vizuri katika Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza Wanawake (WFDL) zikichukua nafasi ya Bilo Queens na Ruangwa Queens zilizoshuka daraja.
Kilimanjaro Wonders ilipanda daraja baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa kuichapa Bunda Girls bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliokuwa na ushindani mkubwa.
Ushindi huo umeifanya timu hiyo ya Kilimanjaro kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya kupitia safari ngumu ya hatua za makundi hadi mtoano.
Safari ya Kilimanjaro haikuwa nzuri sana ilianza hatua ya makundi ikimaliza nafasi ya pili kwenye kundi A ikikusanya pointi tisa nyuma ya Maendeleo Queens iliyomaliza kileleni na pointi 10.
Ikafuzu hatua ya robo fainali ilipoitoa Mlandizi Queens kwa bao 1-0 lililoivusha hatua ya nusu fainali na kuichapa
Maendeleo Queens kwa mabao 2-0 yaliyowavusha kwenda fainali na hatimaye kubeba ubingwa.
Kwa upande wa Bunda Girls ilikata tiketi ya kupanda daraja baada ya kumaliza kileleni mwa kundi C ikiwa na pointi tisa huku Mlandizi Queens ikimaliza nafasi ya pili na pointi sita.
Kwenye hatua ya robo fainali ilitoa Get Program kwa bao 1-0 na kisha kutinga hatua ya nusu fainali ilipoitandika TDS Girls mabao 2-1 kwenye mechi kali na yenye ushindani iliyopigwa Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.
Ilipotinga fainali timu hiyo ilichapwa bao 1-0 dhidi ya Kilimanjaro Wonders iliyobeba taji hilo na kuzifanya timu hizo mbili kucheza ligi kuu msimu ujao ikiwa mara ya kwanza kwao.
Mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 28 kutoka mikoa mbalimbali nchini yalianza Juni 16 jijini Tabora.
Kilimanjaro Wonders na Bunda Girls zilionyesha ubora wao tangu hatua ya makundi hadi mechi za mtoano, jambo lililowezesha kufikia malengo yao ya kucheza Ligi Kuu ya Wanawake.
Mchezaji wa Kilimanjaro Wonders, Vanessa Juma alisema mashindano hayo yamewapa chalenji na walistahili ubingwa kutokana na juhudi walizozifanya.
“Tumekuwa na mashindano mazuri tangu yameanza, mashindano yalikuwa na ushindani mkubwa kwa sababu kwenye timu 28 ni mbili pekee zilikuwa zinatakiwa kupanda hivyo tunashukuru na tumefurahi tunaamini tutafanya vizuri ligi kuu,” alisema Vanessa.
Nahodha wa Bunda, Elizabeth Daniel alisema “Tuliingia kwenye mashindano tukiwa na nidhamu kubwa kwa sababu ni moja ya timu ambayo hatukucheza ligi hivyo lazima uwaheshimu wapinzani wako tunashukuru tutacheza ligi msimu ujao.”