MABAHARI wa KMKM, wamefanikiwa kutetea ubingwa wa Kombe la FA Zanzibar baada ya kuitandika Chipukizi mabao 2-1 katika fainali iliyochezwa Juni 27, 2026 kwenye Uwanja Gombani uliopo kisiwani Pemba.
Mabao mawili yaliyofungwa na Martin Charles, yametosha kuifanya KMKM kutetea ubingwa huo unaowapa nafasi ya kuiwakilisha Zanzibar kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Mbali na KMKM kupata fursa ya kuiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya kimataifa msimu ujao, pia imejinyakulia zawadi ya Sh30 milioni kilichotengwa kwa ajili ya bingwa wa Kombe la FA Zanzibar.
Mchezo huo ulioshuhudiwa na mamia ya mashabiki wa soka, ulijaa ushindani mkubwa kutoka kwa pande zote mbili, huku KMKM ikitumia vyema nafasi chache ilizopata na kufanikiwa kuondoka na ushindi muhimu ulioiwezesha kutwaa taji hilo.
Hii ni mara ya pili timu hizo zinakutana kwenye fainali ya FA na msimu uliopita kwenye Uwanja wa Mao kisiwani Unguja, KMKM ilishinda mabao 4-2 dhidi ya Chipukizi.