
Sheikh Naim Qassim, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, na baadhi ya wabunge wa Hizbullah wamekosoa na kupinga vikali mazungumzo yanayodaiwa kufikiwa kati ya serikali ya Lebanon na utawala haramu wa Israel.
Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alitangaza Ijumaa kwamba baada ya kufanyika mazungumzo huko Washington, mfumo wa makubaliano kati ya Israel na Lebanon tayari ulikuwa umeafikiwa. Katika sherehe ya kusainiwa makubaliano hayo, Rubio alisema kufikiwa mfumo huo wa makubaliano ya awali ndio mwanzo wa kazi kubwa iliyoko mbele. Baada ya Rubio kutangaza habari hii, Hizbullah ilitangaza rasmi kupinga makubaliano hayo ya fedheha. Swali ni kuwa, je, nini kimeipelekea Hizbullah kuchukizwa na kupinga vikali makubaliano hayo ya serikali ya Lebanon na utawala ghasibu Israel ambayo kimsingi yanahatarisha maslahi ya taifa la Lebanon?
Sababu ya kwanza na muhimu zaidi iliyotolewa na Hizbullah ni kwamba, mapatano hayo yanakanyaga wazi misingi ya mamlaka ya kitaifa ya Lebanon na kutoa bure fursa kwa adui Mzayuni. Kwa mtazamo wa Hizbullah, makubaliano yoyote yanapaswa kuulazimisha utawala wa Kizayuni uondoke katika ardhi ya Lebanon unayoikalia kwa mabavu, ambapo katika mapatano ya sasa, utawala wa Kizayuni umeweka sharti la kupokonywa silaha muqawama wa Lebanon, kabla ya kuondoka kwenye ardhi hiyo, suala ambalo Hizbullah hailikubali hata kidogo. Kwa hakika, kwa mtazamo wa Hizbullah, makubaliano yanayodaiwa yanahalalisha ukaliaji mabavu wa Tel Aviv katika ardhi ya Lebanon. Kuhusiana na suala hili, Sheikh Naim Qassim, Katibu Mkuu wa Hizbullah, ameonya kwamba kushurutishwa kuondoka Israel katika ardhi ya Lebanon na kupokonywa silaha muqawama ni kuvuka mistari yote myekundu na kuigeuza Lebanon kuwa chombo cha mchezo mikononi mwa adui. Ameongeza kuwa, kuhalalisha kukaliwa kwa mabavu eneo la kusini mwa Lebanon kunaweza kusababisha ukaliaji wa muda mrefu na hata kunyakuliwa kwa ardhi hiyo na utawala wa Kizayuni.
Sababu nyingine muhimu ni kuwa, Hizbullah inaamini kwamba, serikali ya sasa ya Lebanon iliyoingia madarakani kwa uungaji mkono wa Marekani na utawala wa Kizayuni haina mamlaka wala uhalali wa kisheria wa kufanya mazungumzo na kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni. Hassan Fadhlullah, mwakilishi wa Hizbullah katika bunge la Lebanon, amekosoa makubaliano hayo ya hadaa na kusema kwamba Netanyahu amekuwa akifanya mazungumzo na nafsi yake mwenyewe, kwa sababu serikali ya sasa ya Lebanon haina uhalali wa kikatiba wala uwezo wa kulazimisha matakwa yake.
Sababu nyingine ni kuwa makubaliano haya yanakinzana wazi na makubaliano ya Islamabad kati ya Iran na Marekani. Katika mapatano ya Islamabad, sharti la Iran kuhusu makubaliano yoyote na Marekani ni kusimamishwa mara moja vita vya Israel dhidi ya Lebanon na kuondoka utawala huo ghasibu katika ardhi ya Lebanon, sharti ambalo halijatekelezwa na Israel na kupelekea utawala huo kuwekewa mashinikizo na Marekani. Sasa katika mazungumzo tofauti kati ya Lebanon na utawala wa Kizayuni, Marekani imepuuza sharti hilo na kivitendo imeiacha huru Israel iendelelee kufanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya watu wa Lebanon na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, Hassan Fadhlullah, mbunge wa Hizbullah katika bunge la Lebanon amesisitiza kuwa: “Kilichotokea Washington ni jaribio la kuvuruga njia ya Islamabad, na hakuna makubaliano yoyote kati ya hayo yatakayotekelezwa bila mapambano.” Sheikh Naim Qassim, pia amesema: “Makubaliano ya Washington ni makubaliano ya kufedhehesha, ya aibu na batili, na badala yake vifungu vya maelewano kati ya Iran na Marekani kuhusu kusimamisha vita vya Lebanon vinapaswa kutekelezwa.” Nukta ya mwisho ni kwamba, kwa mtazamo wa Hizbullah, makubaliano ya Washington yameanzishwa kwa shabaha ya kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon kwa sababu makubaliano hayo ambayo yanatilia mkazo kupokonywa silaha na kudhoofishwa Hizbullah yatapelekea makundi ya Lebanon kupigana. Hassan Fadhlullah amesema kuhusiana na suala hilo kuwa, serikali ya sasa ya Lebanon itaweza tu kutekeleza makubaliano hayo yaliyotiwa saini mjini Washington, ikiwa itaungwa mkono na Marekani na hivyo kuisukuma nchi hiyo kwenye hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.