Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni, ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa viwango vya utunzaji wa mazingira katika utendaji wa baadhi ya viwanda nchini.

Miongoni mwa viwanda vilivyofanya vizuri na kupongezwa kwa utekelezaji wa viwango hivyo ni kiwanda cha kuchakata mafuta cha Kamal Refinery, kilichopo Kerege, Bagamoyo mkoani Pwani.

Masauni ametoa kauli hiyo Juni 27, 2026, baada ya kutembelea na kukagua shughuli mbalimbali za kiutendaji katika kiwanda hicho, akiongozana na wataalamu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Katika ziara hiyo, ametembelea maeneo ya uzalishaji na uchakataji wa mafuta ili kujionea mifumo ya uendeshaji wa kiwanda pamoja na hatua zinazochukuliwa kulinda mazingira.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Masauni amekipongeza kiwanda hicho na vingine vinavyotekeleza kikamilifu maelekezo ya mazingira yanayotolewa na NEMC.

“Kuna viwanda vimefanya marekebisho, lakini havijakamilisha, vinaendelea. Kuna viwanda vimefanya vizuri sana na vimekamilisha maelekezo yote kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira,” amesema Masauni.

Amevitaka viwanda vyote nchini kuendelea kuzingatia matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ili kulinda afya za wananchi na kuhakikisha maendeleo ya viwanda yanaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kamal Group of Companies, Satyam Swatantra, ameiomba Serikali kuweka mazingira yatakayowezesha mafuta taka yanayozalishwa nchini kubaki kwa ajili ya uchakataji wa ndani badala ya kusafirishwa nje ya nchi.

“Tunaiomba Serikali iweke mazingira mazuri kuhakikisha malighafi hii inabaki nchini na haisafirishwi kwenda nje ya nchi. Hii itasaidia kuimarisha uchumi wa mzunguko, kuongeza fursa za ajira, kuimarisha viwanda vya ndani na kuhifadhi fedha za kigeni,” amesema.

Meneja wa Miradi wa Kamal Refinery, Prince Mwakimenya, amesema ujio wa Waziri Masauni na wataalamu wa NEMC umeipa kampuni fursa ya kupata ushauri zaidi kuhusu namna ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

“Tunajivunia kuwa tumetekeleza kwa kiwango kikubwa maelekezo yote yaliyotolewa na mamlaka husika, na tutaendelea kuboresha mifumo yetu ya utunzaji wa mazingira,” amesema Mwakimenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *