
Taasisi ya Hind Rajab (HRF) imewasilisha malalamiko kwa Wizara ya Sheria ya Marekani (DoJ), ikitaka kukamatwa na kushtakiwa anayeitwa waziri wa usalama wa taifa wa utawala wa Israel, Itamar Ben-Gvir kwa tuhuma za kutenda jinai.
Ben-Gvir amepanga kutembelea Marekani mwezi ujao, na anatazamiwa kuwasili New York tarehe 7 Julai.
Katika ripoti iliyochapishwa kwenye tovuti yake siku ya Jumamosi, kundi hilo linalowatetea Wapalestina lilieleza kwamba limeiomba Wizara ya Sheria ya Marekani kuanzisha uchunguzi wa makosa ya jinai na kutoa hati ya kukamatwa Ben-Gvir ili kumzuia kuondoka katika mamlaka ya mahakama ya Marekani wakati kesi hiyo ikichunguzwa.
Katika ripoti hiyo, The Hind Rajab Foundation (HRF) imenukuu Sheria ya Uhalifu wa Vita na Sheria ya Mauaji ya Kimbari ya Marekani, ikitaka uchunguzi ufanywe kuhusu idhini ya Ben-Gvir ya kufanyika mateso makali, unyanyasaji wa kinyama, mauaji, ubakaji, unyanyasaji wa kingono, vitendo vya mauaji ya kimbari na uchochezi wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, hasa baada ya vikosi vya jeshi katili la Israel kuanzisha vita dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 2023.
Mwakilishi wa HRF nchini Marekani, Jake Romm, amesema kila nchi duniani ina wajibu wa kumkamata na kumfikisha mahakamani Itamar Ben-Gvir kwa jinai alizofanya.
Romm amesema kuwa Washington, haswa, ina wajibu mkubwa wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Ben-Gvir kwa sababu raia wengi wa Marekani wameteswa mikononi mwake.
“Itamar Ben Gvir ni miongoni mwa wahalifu wakubwa wa zama zetu—mtu anayehusika na kutunga sera ya kikatili ya mauaji, mateso, ubakaji, na unyanyasaji katika mfumo mzima wa magereza ya Israel; mtu anayehusika na kuchochea moja kwa moja mauaji ya kimbari na kutoa amri za kuhakikisha kwamba yanafanyika ardhini; ni mtu ambaye hata mauaji ya miaka miwili na nusu iliyopita hayamtoshi,” amesema mwakilishi wa The Hind Rajab Foundation nchini Marekani, Jake Romm.
“Kila nchi duniani, ikiwa ni pamoja na Marekani, ina wajibu wa kumkamata na kumfikisha mbele ya sheria kwa makosa yake. Zaidi ya hayo, mateso na unyanyasaji wa Ben Gvir kwa raia wa Marekani vinachochea jukumu la kimsingi zaidi la kimamlaka, yaani kuwalinda raia wake” amesema Jake Romm.
Romm amesisitiza kwamba huu ni mtihani wa kipimo cha haki nchini Marekani, kwa ulimwengu kuona kama Washington itatekeleza wajibu wake au la, na je, Marekani inaweza kuaminiwa kwa kushikamana na wajibu wake wa kimaadili wa kutetea haki za binadamu za Wapalestina wasio na ulinzi katika Ukanda wa Gaza, na kwingineko.
Wapalestina wengi, mashirika ya kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali, yamewasilisha ushahidi kwamba chini ya uongozi wa Ben Gvir katika miaka kadhaa iliyopita, vikosi vya jeshi la utawala wa Israel vimekuwa vikiwatesa Wapalestina waliotekwa nyara na kushikiliwa katika korokoro na magereza ya Israel.