
Dar es Salaam. Tafiti mbalimbali zilizofanywa katika Kanda ya Kaskazini na watafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro (KCMC) na washirika wa ndani na nje ya nchi, zimeonesha kuwa magonjwa ya moyo yanaongezeka kwa kasi, huku idadi kubwa ya wananchi wakiishi na magonjwa hayo bila kufahamu au kuyadhibiti.
Akizungumza na Mwananchi jana, Juni 27, 2026 kuhusu ushahidi wa kisayansi uliopo, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti JKCI, Dk Pedro Pallangyo, amesema mpaka sasa kuna tafiti nyingi tofauti zilizofanyika Kanda ya Kaskazini, zilizoangalia magonjwa ya moyo, uelewa wa wananchi na mtindo wa maisha.
“Tumefanya tafiti nyingi, hasa za shinikizo la damu, mishipa ya moyo kuziba, uelewa wa jamii kuhusu sababu hatarishi za magonjwa ya moyo, na uzingatiaji wa mtindo bora wa maisha kuzuia magonjwa ya moyo,” amesema Dk Pedro.
Juni 24, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaagiza watafiti nchini kufanya uchunguzi wa kina kubaini sababu za ongezeko la magonjwa ya moyo na saratani, hususan katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Rais Samia alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa jengo la tiba ya mionzi katika Hospitali ya KCMC, baada ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Mwenyekiti wa Bodi ya KCMC, Dk Alex Malasusa, kueleza kuwa wagonjwa wengi wa moyo wanaofika hospitalini hapo wanatoka katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
“Hapa nimemsikia Askofu Malasusa akisema wenye maradhi ya moyo wanatoka Kaskazini na kwamba tukimalizia jengo lile litasaidia wagonjwa kutokwenda JKCI, watatibiwa hapa,” alisema Rais Samia, akisisitiza kuwa lengo ni kutaka watafiti wabaini sababu za maeneo hayo kuwa na wagonjwa wengi wa moyo.
Moja ya tafiti kubwa ni “Epidemiology of Hypertension in Northern Tanzania: A Community-Based Mixed-Methods Study”, iliyochapishwa mwaka 2017 baada ya utafiti uliofanyika kati ya 2013 na 2015 katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Utafiti huo ulihusisha watu 481 kutoka kaya 346 na ulilenga kubaini kiwango cha shinikizo la damu katika jamii, uelewa wa wananchi kuhusu ugonjwa huo pamoja na changamoto zinazokwamisha matibabu.
Matokeo yalionesha kuwa asilimia 28 ya washiriki walikuwa na shinikizo la damu. Hata hivyo, ni asilimia 48.3 pekee waliokuwa wanajua kuwa wana ugonjwa huo, wakati asilimia 95.3 ya waliokuwa na shinikizo la damu hawakuwa wamelidhibiti.
Utafiti pia ulibaini kuwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na wanaotumia pombe walikuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata shinikizo la damu, huku changamoto kubwa zikiwa uelewa mdogo wa ugonjwa, mawasiliano hafifu kati ya wahudumu na wagonjwa, foleni ndefu na upungufu wa watoa huduma waliofunzwa.
Dk Pallangyo amesema watafiti pia walifanya utafiti wa “Knowledge, Attitudes and Preventive Practices Regarding Ischemic Heart Disease Among Emergency Department Patients in Northern Tanzania” mwaka 2019, uliolenga kupima uelewa wa wananchi kuhusu ugonjwa wa mishipa ya moyo kuziba na hatua wanazochukua kujikinga.
Katika utafiti huo uliowahusisha wagonjwa 349, ilibainika kuwa wananchi wengi hawakutambua dalili muhimu za mshtuko wa moyo.
Aidha, asilimia 46.4 ya washiriki walikuwa na uzito uliopitiliza au unene, huku asilimia 65.3 wakionekana katika hatari ya zaidi ya asilimia 10 ya kupata ugonjwa wa moyo ndani ya miaka mitano ijayo.
Watafiti walihitimisha kuwa elimu kuhusu dalili za mshtuko wa moyo na vihatarishi vyake inahitaji kuimarishwa.
Katika utafiti mwingine wa mwaka 2019 ulioitwa “The Burden of Hypertension and Diabetes in an Emergency Department in Northern Tanzania”, watafiti walichunguza ukubwa wa tatizo la shinikizo la damu na kisukari kwa wagonjwa waliokuwa wakifika katika idara ya dharura.
Matokeo yalionesha kuwa magonjwa hayo mawili yalikuwa miongoni mwa sababu kuu za wagonjwa kuhitaji huduma za dharura, hali iliyosisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mapema na huduma za kinga ili kuzuia madhara ya magonjwa ya moyo.
Aidha, kupitia utafiti wa “The Burden of Acute Coronary Syndrome, Heart Failure and Stroke Among Emergency Department Admissions in Tanzania” uliochapishwa mwaka 2019, watafiti walibaini kuwa moyo kushindwa kufanya kazi ni miongoni mwa sababu kuu za wagonjwa kulazwa hospitalini, huku wagonjwa wengi wakifika katika hatua za mwisho za ugonjwa, jambo linaloongeza hatari ya vifo.
Mwaka 2022, utafiti ulioitwa “Healthcare-Seeking Behaviour, Barriers to Care and Predictors of Symptom Improvement Among Patients with Cardiovascular Disease in Northern Tanzania” ulichunguza namna wagonjwa wa magonjwa ya moyo wanavyotafuta matibabu na vikwazo vinavyowakabili.
Utafiti huo ulibaini kuwa wagonjwa wengi huchelewa kufika hospitalini kutokana na gharama za matibabu, umbali wa vituo vya huduma na uelewa mdogo kuhusu dalili za awali za magonjwa ya moyo.
Watafiti walionya kuwa kuchelewa huko kunachangia wagonjwa wengi kufika wakiwa tayari wanahitaji matibabu ya kibingwa au upasuaji.
Katika utafiti wa mwaka 2023 uliopewa jina “Prevalence of Hypertension and Associated Factors Among Diabetic Patients in Kilimanjaro Region”, watafiti walichunguza kiwango cha shinikizo la damu kwa wagonjwa wa kisukari.
Utafiti uliowahusisha wagonjwa 315 ulibaini kuwa asilimia 55.2 walikuwa pia na shinikizo la damu. Hatari ilikuwa kubwa zaidi kwa wagonjwa wenye umri zaidi ya miaka 60, wenye historia ya ugonjwa wa mishipa ya moyo na wavutaji sigara. Watafiti walipendekeza wagonjwa wote wa kisukari wapimwe shinikizo la damu kila wanapofika kliniki.
Dk Pallangyo amesema tafiti hizo zimeonesha wazi kuwa mzigo wa magonjwa ya moyo unaongezeka Kanda ya Kaskazini, huku vihatarishi vikuu vikiwa shinikizo la damu, kisukari, unene kupita kiasi, matumizi ya pombe, kutofanya mazoezi na kuchelewa kufanya uchunguzi wa afya.
Amesema matokeo hayo yamekuwa msingi wa JKCI na KCMC kuimarisha kampeni za uchunguzi wa mapema, elimu kwa umma na upanuzi wa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo ili kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza.
Tafiti zinaendelea
Hata hivyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa KCMC, Dk Gissela Nyakunga, amesema ili kupata majibu ya kisayansi kuhusu sababu zinazoifanya Kanda ya Kaskazini kuongoza kwa wagonjwa wa valvu za moyo wanaohitaji upasuaji, KCMC inaendelea na utafiti maalumu ambao bado haujakamilika.
Amesema ni mapema kuhusisha hali hiyo na sababu yoyote bila ushahidi wa kisayansi, ingawa baadhi ya wagonjwa wanaweza kuwa wameathiriwa na magonjwa ya kuambukiza yanayosababisha kuharibika kwa valvu za moyo.
“Hatupaswi kutoa hitimisho kabla ya utafiti kukamilika. Tunahitaji ushahidi wa kisayansi ili kujua kwa nini wagonjwa wengi wa aina hii wanatoka Arusha,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Nyakunga, hali ni tofauti kwa wagonjwa wenye magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo, ambao wengi wao hutoka mkoani Kilimanjaro, hasa Moshi. Amesema magonjwa hayo kwa kiasi kikubwa yanahusishwa na mtindo wa maisha unaojumuisha ulaji usiofaa, kutofanya mazoezi, unene uliopitiliza, shinikizo la damu na kisukari.
Amesema huduma za upasuaji wa mishipa ya damu ya moyo bado zinapatikana JKCI, hivyo KCMC huwapa rufaa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo, ingawa ni takribani asilimia 10 pekee ya wagonjwa wanaopokelewa hospitalini hapo.
“Wagonjwa wengi wanaofanyiwa upasuaji JKCI hufika moja kwa moja kutoka Arusha, Manyara na mikoa mingine. Baada ya matibabu hurudi KCMC kwa ajili ya ufuatiliaji wa afya zao katika kliniki zetu,” amesema Dk Nyakunga.