Musoma. Wakati Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akitarajiwa kufanya ziara ya siku tano mkoani Mara, baadhi ya wakazi wa mkoa huo wamesema wanatarajia ziara hiyo itasaidia kutatua changamoto ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa ya kimkakati.

Katika ziara hiyo inayotarajiwa kuanza Julai 1 hadi 5, 2026, Dk Mwigulu atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo, sambamba na kuzungumza na wananchi na kusikiliza kero zao.

Wakizungumza mjini hapa leo Jumanne Juni 30, 2026, wakazi hao wamesema ipo miradi mikubwa ambayo utekelezaji wake umekuwa ukisuasua, hivyo ziara hiyo kwa namna moja ama nyingine inapaswa kusaidia ukamilishaji wa miradi hiyo ili kuendelea kuinua uchumi wa mkoa na watu wake.

Wametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kadhaa ndani ya mkoa huo ikiwemo barabara ya Tarime – Mugumu, Sanzate – Mugumu, Musoma – Busekekela na Mika –Kirongwe, barabara ambazo ujenzi wake umekuwa ukisuasua huku sababu ikielezwa kuwa ni ukosefu wa fedha.

“Hizo barabara zinashikilia uchumi wa mkoa, lakini ujenzi wake umekuwa wa kusuasua, tunaomba katika ziara hii tupate majibu ambayo yanaendana na ukamilishaji wake ili uchumi wa mkoa ukue zaidi,” amesema Joshua Bwana.

Bwana amesema ujenzi wa bandari ya Musoma pia, ni jambo ambalo wakazi hao wanasubiri kusikia kauli ya kiongozi huyo, amesema ingawa zipo ahadi kadhaa zimetolewa kuhusu bandari hiyo lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea.

Musa Mafuru amesema ubovu wa miundombinu hasa ya barabara katika maeneo ya vijijini ni suala ambalo wanatarajia kusikia kauli ya Serikali ili kuona namna gani changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi

“Sio kwamba viongozi waliopo hapa wameshindwa kutatua changamoto hizo, lakini unajua mkubwa ni mkubwa tu, yawezekana kuna mambo hayaendi lakini yeye akitoa maagizo lazima yatatekelezwa kwa wakati,” amesema.

Bwana amesema kutokana na mvua zilizonyesha, barabara nyingi za mkoa huo hususan zilizopo maeneo ya vijijini zimeharibika, hivyo wanaamini ujio wa waziri huyo utakwenda sambamba na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo.

Joel Ndege amesema wakazi wa mkoa huo wanatarajia kuanza kunufaika na safari za ndege za ATCL kuanzia mwezi ujao kwa mujibu wa ahadi iliyotolewa na Waziri wa Uchukuzi mapema mwezi huu wakati wa majaribio ya kuruka na kutua kwa ndege katika uwanja wa Musoma, lakini ujenzi wa uwanja huo bado haujakamilika kwa asilimia 100.

“Tunafurahi kuwa sasa ndege kubwa zinatarajiwa kuanza kutoa huduma kwenye uwanja wetu lakini uwanja ule bado haujakamilika, pia, hakuna jengo la kudumu la abiria kwa hiyo tunatarajia Waziri Mkuu ataelekeza jambo lifanyike na kama unavyojua huyu ni kiongozi mkubwa kwenye nchi yetu lazima agizo lake litekelezwe kwa wakati,” amesema Ndege.

Kwa upande wake, Asia Manumbu amesema wanatarajia kusikia mikakati ya kufufua viwanda, kujenga vingi kwa maelezo kuwa licha ya mkoa huo kuwa na rasilimali za kutosha lakini bado hakuna viwanda.

“Huwezi kuinua uchumi wakati hatuna viwanda, tunatarajia hili nalo litapata kauli ua Serikali kwani kwenye viwanda mbali na kuinua uchumi wa mkoa lakini kutakuwa na fursa za ajira hivyo kuboresha pato la mtu mmoja mmoja na jamii nzima,” amesema.

Ameongeza kuwa changamoto ya upatikanaji wa maji hasa katika maeneo ya vijijini, pia, ni jambo ambalo wakazi wa mkoa huo wanaamini kuwa itapatiwa ufumbuzi kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema Dk Mwigulu anatarajiwa kufanya ziara hiyo mkoani humo kuanzia Julai Mosi hadi tano mwaka huu.

Kanali Mtambi amesema katika ziara hiyo, Waziri Mkuu anatarajiwa kukagua, kutembelea na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh52.9 bilioni miradi iliyopo kwenye sekta za afya,elimu, miundombinu, utawala na maji.

Amesema akiwa mkoani Mara Dk Mwigulu anatarajiwa kufanya ziara katika halmashauri zote tisa za mkoa huo na katika majimbo yote 10 ya uchaguzi ambapo pamoja na mambo mengine atasikiliza na kutatua kero za wananchi.

“Nitoe wito kwa wana Mara wote kutumia fursa hii kujitokeza kumlaki na kusikiliza ujumbe alionao kiongozi wetu kwao, pia kupitia ziara hii kero za wananchi zitasikilizwa na kutatuliwa kama ambavyo Serikali imekuwa ikifanya ili kuondokana na kero za wananchi,” amesema na kuongeza

“Uongozi wa mkoa wa Mara tunaitizama  ziara hii kama kichocheo cha  maendeleo kwani mbali na kukagua miradi lakini pia atatumia fursa hiyo kusikiliza kero ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaweza kuwa sababu ya kuchelewesha maendeleo yetu, ujio wa waziri mkuu ni faraja kwa wana Mara,”

Amesema wakati wa ziara hiyo, Dk Mwigulu atakagua miradi hiyo ya maendeleo katika wilaya zote sita sambamba na kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali katika halmashauri zote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *