Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesema kuwa sherehe za kitaifa za kuaga na mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, zitatumika kama jukwaa la harakati za kimataifa za kulaani ugaidi na maandamano hai dhidi ya jinai zinazofanywa na mhimili wa Marekani na Uzayuni.

Brigedia Jenerali Mohammad Akrami-Nia, msemaji wa Jeshi hilo, ametoa kauli hiyo siku ya Jumanne, huku akifafanua maandalizi ya Jeshi kwa ajili ya hafla hiyo ya kitaifa.

Sherehe za kumwaga Shahidi Imam Khamenei kwa umma zitafanyika tarehe 4 na 5 Julai katika Ukumbi wa Swala wa Imam Khomeini, ikifuatiwa na misafara ya mazishi jijini Tehran na Qom tarehe 6 na 7 Julai. Mwili wa Kiongozi huyo Shahidi utazikwa tarehe 9 Julai katika Haram ya Imam Ridha (AS) mjini Mashhad.

Akrami-Nia alieleza kuwa mazishi hayo yana uzito unaovuka mipaka ya tukio la kitaifa, akiongeza kuwa wananchi wa Iran, kama watu wenye shukrani na utiifu kwa uongozi wa taifa, wakishirikiana na wafuasi wa Kiongozi huyo Shahidi kutoka mataifa mengine, wataandika “shairi kubwa la kihistoria” wakati wa hafla hiyo.

Amesema Jeshi, kwa kuendeleza utekelezaji wa wajibu wake, litashiriki katika “uwepo huo wa kishujaa” wa taifa wakati wa hafla ya kuaga, akibainisha kuwa kikosi hicho kimekamilisha maandalizi makubwa ya kusaidia kufanikisha sherehe hizo.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, Jeshi limejiandaa kuchangia katika kulinda usalama wa taifa, kutoa huduma kwa umma, na kutekeleza majukumu ya kisherehe yanayohusiana na mapokezi ya wageni wa kkimataifa watakaohudhuria hafla hiyo.

Msemaji huyo pia ametangaza kuimarishwa kwa hatua za kiusalama katika mipaka ya nchi kavu na anga ya Iran kabla ya hafla hiyo.

Amesema vikosi vya ziada vya Jeshi la Nchi Kavu vimepelekwa kuimarisha usalama mipakani, huku Jeshi la Ulinzi wa Anga likiendelea kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa anga ya Iran ili kuimarisha usalama wa anga na kudhibiti usafiri wa anga nchini katika kipindi hiki cha ongezeko la safari za ndege za kimataifa na kuvuka mipaka.

Akrami-Nia ameongeza kuwa Jeshi la Anga na Jeshi la Majini pia viko katika hali ya tahadhari kamili ya kiutendaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *