
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr al-Busaidi, ametangaza msimamo wa nchi yake kuunga mkono mpango wa Iran wa kuanzisha utaratibu wa “ada za huduma za baharini” kwa meli zinazopita katika Lango Bahari la Hormuz.
Katika mahojiano na shirika la utangazaji la Monte Carlo Doualiya, yaliyochapishwa rasmi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman siku ya Jumatatu, Bwana al-Busaidi amesisitiza tena utiifu wa Muscat kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (UNCLOS).
Waziri huyo alifafanua bayana kuwa Oman inapinga vikali tozo zozote zinazohusiana na haki ya kupita kwa meli. Hata hivyo, amebainisha tofauti muhimu kati ya tozo za kupita na ada halali za huduma za baharini, ikiwemo utunzaji wa mazingira na usalama wa urambazaji, ambazo zinaweza kujadiliwa kwa hiari kati ya Iran na nchi au makampuni yanayonufaika na huduma hizo.
Waziri al-Busaidi amesema kuwa ada kama hizo zingechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha usalama wa usafirishaji, kulinda maji hayo dhidi ya uchafuzi, na kuboresha utayari wa kukabiliana na ajali au dharura za baharini; akitolea mfano wa mifumo ambayo tayari inatekelezwa kwa mafanikio katika Lango la Malacca na maeneo yanayozunguka Singapore.
Amesisitiza kuwa Oman na Iran zimekubaliana kikamilifu kuwa makubaliano yoyote yajayo kuhusu lango hilo lazima yabaki ndani ya mipaka na mfumo wa sheria za kimataifa.
Kuhusu mapendekezo ya Ufaransa na Uingereza ya kusafisha migodi katika njia hiyo ya maji, Bwana al-Busaidi amesisitiza kuwa jukumu kuu la kuhakikisha usalama wa lango hilo na njia za kimataifa za meli ni la Iran, kwa mujibu wa mkataba wa maelewano (MoU) uliotiwa saini hivi karibuni kati ya marais wa Iran na Marekani.
Kauli zake zinakuja kufuatia mkutano wa kwanza wa kamati ya pamoja ya Iran na Oman kuhusu Lango la Hormuz, ambayo imejikita katika kujadili utawala na uendeshaji wa lango hilo hapo baadaye.
Ikumbukwe kuwa Iran ilifunga Lango la Hormuz kwa maadui zake na washirika wao kufuatia wimbi la karibuni la uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Mkataba wa maelewano uliopatanishwa na Pakistan hivi karibuni uliotiwa saini kati ya Tehran na Washington unalenga kukomesha mzunguko huo wa uhasama.
Chini ya makubaliano hayo yenye vipengele 14, Iran inatakiwa kuhakikisha kuwa meli za kibiashara zinapita bila tozo yoyote kwa muda wa angalau siku 60, huku kukiwa na urejeshaji kamili wa mzunguko wa meli katika Lango la Hormuz ndani ya siku 30. Kipengele cha tano cha mkataba huo kinatambua wazi mamlaka ya Iran juu ya njia hii muhimu ya kimkakati.