
Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon ametahadharisha kuhusu njama mpya dhidi ya Lebanon akiashiria makubaliano ya Washington kati ya serikali ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwahutubu wananchi wa nchi hiyo kwa kusema: “Enyi watu wa Lebanon, hii ni njama hatari.”
Makubaliano ya Washington kati ya Lebanon na utawala wa Kizayuni yalitiwa saini Ijumaa iliyopita. Wakati makubaliano hayo yanadai kudhamini na kulinda mamlaka ya Lebanon, yanataka kupokonywa silaha harakati ya mapambano ya kupigania ukombozi wa Lebanon. Isitoshe, mara tu baada ya kusainiwa mapatano hayo, Netanyahu alitangaza kwamba Israel itasalia katika “eneo la usalama” la kusini mwa Lebanon na kuwa haitaruhusu watu waliohamishwa kwa nguvu kurudi makwao. Makubaliano hayo pia yana vifungu vingine vinavyoendana na maslahi ya Israel na ahadi ndogo tu kuhusu kuimarishwa uchumi wa Lebanon.
Swali ni kuwa, je, kwa nini makubaliano ya Washington yanalenga kufungua njia ya fitna mpya nchini Lebanon?
Jambo la kwanza ni kuwa sio tu kwamba hakuna msimamo mmoja nchini Lebanon kuhusu makubaliano hayo, bali pia yameibua mgawanyiko mkubwa nchini kuhusu suala hilo. Hizbullah imeyataja kuwa ya “kufedhehesha” na yasiyo halali, huku Harakati ya Amal ikiyaona kuwa kinyume na maslahi ya kitaifa ya Lebanon. Chama cha Free National Movement, kinachoongozwa na Gebran Bassil, pia kimekosoa vipengele vya makubaliano hayo na kusema vinaweza kuendeleza uvamizi wa Israel nchini humo. Jumuiya ya Kiislamu, Baraza la Wanazuoni wa Kiislamu, Chama cha Kitaifa cha Kisoshalisti, Chama cha Kikomunisti, na wanasiasa mashuhuri, Talal Arslan na Walid Jumblatt pia wamekosoa vifungu vya makubaliano hayo, wakivichukulia kuwa tishio kwa mamlaka na uthabiti wa Lebanon.
Kinyume chake, Chama cha Vikosi vya Lebanon kinachoongozwa na Samir Geagea, Chama cha Kataeb kinachoongozwa na Sami Jamil, na idadi ya wawakilishi walio karibu na nchi za Magharibi wameunga mkono makubaliano hayo, wakidai kuwa ni hatua ya kuelekea utulivu wa Lebanon na kumaliza mvutano wa silaha na Hizbullah. Tovuti ya an-Nashra imeandika kuhusiana na hili kwamba: “Mpasuko mkubwa umeibuka nchini Lebanon kuhusu waraka huu. Serikali, ikiwakilishwa na Rais Joseph Aoun na timu yake inayomuunga mkono, wanaona makubaliano haya kama njia isiyoepukika na ya pekee katika kusimamisha uharibifu wa kimfumo na wala hawaoni tatizo lolote katika kutoa mhanga silaha za Hizbullah, ambazo zimeilinda Lebanon kwa miongo kadhaa, katika kujaribu kuokoa mfumo wao wa kisiasa nchini. Katika upande wa pili, mrengo unaoiunga mkono Hizbullah na washirika wake wanapinga vikali mchakato huu, ikizingatiwa kuwa ni hati ya kuisalimisha Lebanon na kuikabidhi kwa mikono miwili kwa maadui zake, jambo ambalo linavuruga mlingano wake wa kuzuia hujuma ya adui. Wanachukulia utekelezaji wa makubaliano hayo kama kamari hatari kwa umoja wa ardhi ya Lebanon.”
Jambo jingine ni kwamba, makubaliano ya Washington yanasisitiza ulazima wa kupokonywa silaha muqawama wa Lebanon kabla ya kuondoka wanajeshi vamizi wa Israel nchini Lebanon, na pia eti kwa ajili ya kuboresha hali ya uchumi wa nchi hiyo. Tovuti ya an-Nashra inasema: “Makubaliano haya yanajitambulisha kama mdhamini wa uhuru wa Lebanon na uondokaji wa jeshi la Israel nchini, lakini mantiki hii inakabiliwa na dosari kubwa ya kimuundo; kwa sababu kifungu cha 2 kinaambatanisha waziwazi uondokaji huo na “upokonywaji silaha wa makundi yenye silaha” na kubomolewa miundombinu yao. “Sharti hili lisilowezekana” linalitaka jeshi la Lebanon kufanya jambo ambalo jeshi la Israel lenyewe limeshindwa kulifanya. Kwa kuwa upokonyaji silaha wa hiari wa Hizbullah linaonekana kuwa jambo lisilowezekana, kifungu hiki kinaipa Tel Aviv udhuru wa kisheria na wa dhahabu wa kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon.” Kwa kweli, fitina mpya katika makubaliano haya ni kutambuliwa rasmi uvamizi wa Israel nchini Lebanon. Jambo la tatu ni kwamba, kutokana na mgawanyiko wa wazi na mkubwa uliojitokeza huko Lebanon kuhusu makubaliano hayo, kuna uwezekano pia wa kuibuka mizozo ya ndani, jambo ambalo Nabih Berri ametahadharisha wahusika kuhusiana nalo. Spika huyo wa Bunge la Lebanon amesisitiza kuwa: “Hatari kuu ya mapatano haya ni kuibuliwa migawanyiko ya ndani na kuwafanya Walebanoni wapigane wao kwa wao, jambo ambalo litainufaisha moja kwa moja Israel. Makubaliano haya ni fitna ambayo inatishia umoja wa Lebanon na watu wake, na ninapoelezea makubaliano haya kuwa ni ‘uchochezi,’ hili ni onyo la juu kabisa kisiasa.”
Ni kwa sababu hizi ndio maana tovuti ya jarida hilo inahitimisha katika uchambuzi wake kwa kusema: “Mkataba huu wa pande tatu hauwezi kuchukuliwa kuwa mpango endelevu wa amani, bali ni toleo la bomu la muda nchini Lebanon ambalo linaipa Israel ruhusa ya kuendelea na uvamizi wake na kuipa serikali ya Marekani ushindi wa vyombo vya habari, na wakati huo huo kuiweka Lebanon katika makutano ya njia mbili hatari za ima kukubali migogoro ya ndani au ikaliwe kwa mabavu daima.”