Dar es Salaam. Wakati kesho Jumatano, Julai mosi, 2026 agizo la daladala zinazofanya safari barabara ya Kilwa kutoshusha abiria kwenye vituo hadi zifike mwisho wa safari likianza kutekelezwa, wenye daladala hizo wamepewa ahueni.

Hii ni baada ya kuruhusiwa kupita njia nyingine ambazo hazitagusa mradi wa mabasi yaendayo haraka, maarufu kama mwendokasi.

Juni 15, 2026, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) ilitangaza kuwa kuanzia Julai mosi mwaka huu, daladala zote zinazotumia barabara ya Kilwa hazitaruhusiwa kutoa huduma katika maeneo yanayohudumiwa na mradi wa mabasi yaendayo haraka.

Kwa mujibu wa Latra, wananchi wanaotoka Mkuranga, Toangoma na vitongoji vingine, daladala zitakuwa zikiishia kituo cha Mwendokasi cha Mbagala Rangi Tatu, na abiria watatakiwa kuunganisha safari zao kwa kutumia mwendokasi kwenda katikati ya jiji na maeneo mengine.

Uamuzi huo wa Latra unakuja miezi mitatu tangu mtoa huduma wa mabasi hayo, Kampuni ya Mofat, ilalamike kukosa faida ya uwekezaji wake, akisisitiza uwepo wa daladala unafanya mabasi yake kutoa huduma chini ya uwezo wake.

Akizungumza leo Jumanne, Juni 30, 2026, na Mwananchi kuhusu utekelezaji huo, Kaimu Meneja wa Leseni wa Latra, Ngereza Patel amesema ahueni hiyo waliitoa baada ya kukaa kikao na wadau mbalimbali wanaoguswa na agizo hilo, wakiwemo wasafirishaji.

Patel amesema katika kikao hicho, wasafirishaji magari hayo sasa yataruhusiwa kwenda mjini kwa masharti.

Kwa yale ya Mkuranga, Mwandege, Kisemvule, Toangoma na maeneo mengine ya upande huo, yakishashusha abiria Mbagala, yataweza kuendelea na safari kwa kupita kwenye miundombinu ya barabara za mwendokasi bila kushusha abiria hadi mwisho wa safari yake.

Huku pendekezo la pili ni kwa abiria watakaopenda kuendelea kutumia usafiri huo mpaka mjini, basi gari hizo zitakapofika Mbagala na kushusha abiria, zitapita Kilungule Buza, kwenda Tandika, Usalama na kisha kutokea Chang’ombe hadi Gerezani au Machinga Complex.

Pia, walitoa mapendekezo mengine kwamba inawezekana wakishatoka maeneo hayo ya pembezoni wakaingilia Toangoma kisha Kigamboni kupitia Daraja la Kigamboni, mpaka Uwanja wa Taifa, halafu Chang’ombe na kuingia mjini.

“Hili tuliwaambia hamna shida, sababu lengo letu ni sehemu ambayo barabara iliyoboreshwa kwa ajili ya mabasi yaendayo haraka imekamilika na mabasi yameshaanza kufanya kazi, lazima yasogezwe ili kupisha mradi uendelee na shughuli zake.

“Kwa hiyo, kama atataka atumie miundombinu hiyo kwa kwenda sambamba na mabasi yaendayo haraka, asishushe katikati kwa sababu tunataka tuondokane na msongamano,” amesema meneja huyo.

Amesema kutumia njia hizo za mchepuko kwa daladala hizo hakusaidii tu kuondoa msongamano, bali pia zitawasaidia wananchi wa maeneo hayo kupata usafiri kirahisi kwa maeneo ambayo hakuna usafiri wa mabasi ya mwendokasi.

Hata hivyo, amesema si lazima daladala zote kufuata hilo, ni uamuzi wao wanaona ipi rahisi kwao, aidha kuishia Mwendokasi Mbagala au kuendelea na safari.

Kwa upande wa daladala zinazofanya safari zake Mbagala–Mbezi na Mbagala–Gongolamboto, Patel amesema zina machaguo matatu. Ukiacha kupita kwenye miundombinu ya mwendokasi bila kushusha abiria katikati, zinaweza kupita Kilungule, kisha Buza na kutokea Jet Lumo kisha kushika Barabara ya Nyerere.

Barabara nyingine wanayoweza kupita mabasi hayo ni ile ya Kilungule–Buza, kutokea Usalama kwenda Barabara ya Mandela.

Wakitoa maoni yao, mmoja wa wamiliki wa daladala, Ghalib Mohammed, amesema hayo ndiyo yalikuwa mawazo yao tangu awali, lakini walishangaa siku Latra walipotoa tangazo la kutaka gari zote ziishie Mbagala au kutoshusha abiria barabarani.

Mohammed amesema kwao wanaona itazidi kuwasogezea huduma wananchi, lakini pia wamiliki kuwa na uwanja mpana wa kufanya biashara hiyo kwa kuwa sasa wameongezewa njia za kupita.

Mmiliki mwingine wa daladala, Break Salim Break, amesema ni vema biashara huria ikaachwa ifanyike kwa uhuru, ambapo mwenye uwezo wa kupanda mwendokasi atafanya hivyo na yule mwenye uwezo wa kupanda daladala atafanya hivyo pia.

“Kama ni mikopo katika kununua magari, anayelipa mwekezaji wa mwendokasi hata sisi tunachukua mikopo, sasa iweje yeye aonekane ndiye anaumia kuliko sisi, waache biashara huria ifanye kazi yake,” amesema Break.

Naye dereva aliyejitambulisha kwa jina la Fredrick Kajuna, amesema wanaiona hasara ya mafuta watakayopata katika mizunguko ya barabara zilizoorodheshwa kama mbadala wa kuikwepa BRT (mradi wa mabasi yaendayo haraka).

Baadhi ya wananchi, akiwemo Efracia John, mkazi wa Kigamboni, amesema maamuzi hayo kwao ni furaha ukizingatia njia hiyo hakuwa na mabasi ya ruti nyingi, jambo lililowalazimu kupanda magari matatu wanapohitaji kwenda sehemu.

Gabriel Kimondo, mkazi wa Toangoma anayefanya shughuli zake kwa Azizi Ally, amesema hali hiyo itawaumiza wale wanataka kushuka katikati, lakini kwa kuwa ndiyo maagizo ya serikali hawana budi kuyatii.

Kwa upande wake, Asha Abdallah amesema katika masharti hayo mapya atafurahi kama nauli itakuwa ileile waliyokuwa wakipanda awali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *