BAADA ya kufanya tathmini ya kina kuhusu mradi wa Yanga, aliyekuwa kocha wa Raja Casablanca ya Morocco, Fadlu Davids ameridhia kujiunga na mabingwa hao wa Kihistoria Ligi Kuu ya NBC kwa makubaliano ya awali.
Makubaliano hayo ni kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine kulingana na mafanikio ya timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata kutoka kwa mtu wa karibu na Fadlu, pande hizo zimefikia hatua nzuri baada ya siku kadhaa za majadiliano yaliyohusisha masuala ya mshahara, benchi la ufundi, mazingira ya kazi na malengo ya muda mrefu ya klabu.
“Makubaliano makubwa yamefikiwa, kilichobaki ni kukamilisha baadhi ya taratibu za mwisho na maandalizi ya kusaini, Fadlu ameridhishwa na maono ya Yanga na ameonyesha utayari wa kuanza kazi,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Yanga imempa Fadlu ofa ya mshahara wa dola 19,000 kwa mwezi ambapo ni zaidi ya Sh49.8 milioni, sambamba na nyumba ya kuishi pamoja na familia yake, gari la kutembelea na tiketi za ndege kwa matumizi yake binafsi ikiwa atahitaji kusafiri nje ya Tanzania.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba, kocha huyo ameweka wazi kuwa angependa kufanya kazi na sehemu kubwa ya benchi lake la ufundi alilozoea, jambo ambalo Yanga imelipokea kwa mikono miwili kwani inaaminika itasaidia kuharakisha utekelezaji wa falsafa yake ya soka.
“Ametoa majina ya watu anaotaka kufanya nao kazi, miongoni mwao yupo (Abdihamid) Moallin ambaye tayari amekubali kuwa sehemu ya benchi hilo pia atakuja na wasaidizi wengine aliokuwa akifanya nao kazi tangu alipokuwa Simba kabla ya kwenda Morocco,” kiliongeza chanzo hicho.
Moallin ndiye kaimu kocha mkuu wa Yanga aliyemaliza msimu kwa kuipa taji la Ligi Kuu Bara kufuatia timu hiyo kuachana na Pedro Goncalves miezi michache iliyopita.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa, bado kuna hatua za mwisho za kisheria na maandalizi ya nyaraka kabla ya klabu kutangaza rasmi ujio wa kocha huyo, ingawa hakuna tofauti kubwa iliyobaki kati ya pande hizo.
Mmoja wa viongozi wa karibu na mchakato huo amesema viongozi wa Yanga wanaamini Fadlu ndiye aina ya kocha anayefaa kuendeleza mradi wa timu hiyo kutokana na uwezo wake wa kujenga timu zenye ushindani mkubwa, nidhamu ya kiufundi na uelewa wake wa mazingira ya soka la Afrika Mashariki.
“Anaijua vizuri ligi ya Tanzania, anaijua presha ya Simba na Yanga, ana uzoefu wa mashindano ya CAF na ana uwezo wa kuboresha wachezaji mmoja mmoja, hivyo viongozi wanaamini anaweza kuendeleza mafanikio yaliyopo,” amesema mtoa taarifa huyo.
Kama dili hilo litakamilika, Yanga itakuwa imefanikiwa kumshawishi mmoja wa makocha wenye rekodi nzuri barani Afrika katika misimu miwili iliyopita.
Kabla ya kutua Simba, Fadlu alikuwa kocha msaidizi wa Raja Casablanca chini ya Josef Zinnbauer ambapo walitengeneza historia kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Morocco (Botola Pro) msimu wa 2023-2024 bila kupoteza mchezo hata mmoja.
Mbali na ubingwa huo, Raja ilitwaa pia Kombe la Throne na kukamilisha mataji mawili makubwa ya ndani huku Fadlu akitajwa kuwa mmoja wa watu muhimu katika maandalizi ya kiufundi, uchambuzi wa wapinzani na maendeleo ya kikosi.
Mafanikio hayo ndiyo yaliyomfungulia mlango wa kupewa kazi ya ukocha mkuu Simba mwanzoni mwa msimu wa 2024-2025, licha ya kuwa msimu wake wa kwanza kama kama kocha mkuu nchini Tanzania, aliibadilisha Simba haraka na kuifanya kuwa moja ya timu zenye ushindani mkubwa ndani na nje ya nchi.
Akiwa Simba, Fadlu alikiongoza kikosi hicho kucheza mechi 36 za mashindano tofauti, akishinda 26, sare sita na kupoteza nne pekee, rekodi iliyompa wastani wa zaidi ya asilimia 72 ya ushindi.
Rekodi yake kubwa zaidi ilisimama katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo aliiongoza Simba kucheza fainali ya mashindano hayo ambapo ilipoteza dhidi ya RS Berkane, mechi ya kwanza ugenini ilifungwa mabao 2-0 huko Morocco, nyumbani ikawa sare ya bao 1-1.
Utendaji huo ndiyo uliifanya Raja Casablanca kumrejesha Fadlu nchini Morocco, safari hii si kama kocha msaidizi bali kocha mkuu, uongozi wa Raja uliamini alikuwa ameiva vya kutosha kuiongoza moja ya klabu kubwa zaidi Afrika baada ya mafanikio aliyoyapata Tanzania.
Hata hivyo, safari yake ya pili ndani ya Raja Casablanca haikuwa ndefu kutokana na presha kubwa ya matokeo inayozunguka moja ya klabu kubwa zaidi nchini Morocco, katika kipindi cha takribani miezi tisa alichokinoa kikosi hicho, Fadlu alikiongoza Raja katika mechi 22 za mashindano yote, akishinda 13, kutoka sare tano na kupoteza nne, ikiwa ni wastani wa karibu asilimia 59 ya ushindi na pointi 1.86 kwa kila mechi.