Unguja. Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imekusanya Sh1.215 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni asilimia 96.7 ya lengo la kukusanya Sh1.257 trilioni.

Makusanyo hayo ni ongezeko la Sh353.841 bilioni ikilinganishwa na Sh861.882 bilioni zilizokusanywa katika mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ukuaji wa asilimia 41.05.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Julai 2, 2026 na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa ZRA, Makame Khamis Moh’d, ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi pamoja na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Amesema uwekezaji uliofanywa katika ujenzi wa miundombinu na utoaji wa huduma za kijamii, sambamba na utekelezaji wa sera nzuri za kiuchumi, umechangia kuimarika kwa mazingira ya biashara na kuongeza mapato ya Serikali.

Aidha, amesema kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kunakochangiwa na sera na uongozi wa viongozi wa pande zote za Muungano, kumeimarisha mazingira ya biashara na kuongeza mapato ya kodi.

Makame amesema sababu nyingine ni kuunganishwa kwa mifumo ya biashara ya walipakodi na mifumo ya ZRA, hususan katika sekta ya hoteli za kitalii, hatua ambayo imeongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato.

Pia amesema mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya kodi kupitia matumizi ya teknolojia na kambi za huduma zinazowafikia wafanyabiashara katika maeneo yao ya biashara.

Ametaja mikakati mingine iliyochangia mafanikio hayo kuwa ni kuongezeka kwa usajili wa walipakodi wapya, wakiwemo wafanyabiashara wa kimataifa wanaofanya biashara Zanzibar, pamoja na kuimarika kwa ushirikiano kati ya ZRA na walipakodi.

“Kuimarika kwa uwajibikaji na weledi wa watumishi wa ZRA kumeongeza uthabiti katika usimamizi na ukusanyaji wa mapato,” amesema Makame.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, ZRA imepewa jukumu la kukusanya Sh1.726 trilioni.

Ili kufikia lengo hilo, Makame amesema mamlaka hiyo imejipanga kuongeza kasi ya kuunganisha mifumo ya biashara ya walipakodi na mifumo ya ZRA ili kuiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi za biashara na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Amesema pia ZRA itaimarisha uhakiki wa taarifa za bidhaa zinazoingia Zanzibar kupitia mifumo ya kidijitali kwa lengo la kuongeza mapato yatokanayo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) pamoja na ushuru wa bidhaa.

“Vilevile, tutaendelea kutoa elimu na huduma za kodi kwa ukaribu zaidi kupitia kambi za huduma katika maeneo ya biashara ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa walipakodi wa makundi mbalimbali,” amesema.

Kwa mujibu wa Makame, mamlaka hiyo pia itaongeza usimamizi wa ukaguzi wa walipakodi, kuimarisha ushirikiano na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali katika kubadilishana taarifa za kibiashara, pamoja na kufuatilia miradi yote ya Serikali inayotekelezwa ili kuhakikisha kodi stahiki zinazotokana na miradi hiyo zinakusanywa ipasavyo.

Aidha, amesema ZRA itaendelea kutumia mifumo ya kidijitali katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi ya zuio kwa lengo la kuongeza ufanisi na uwazi katika ukusanyaji wa mapato.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *