Ripoti mpya ya Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel imefichua mwelekeo mpya wa vita kwa kuwasilisha ushahidi wa kulengwa kimfumo watoto wachanga huko Gaza.

“Unapompiga risasi kichwani mtoto mchanga wa siku kumi, hakuna hoja yoyote inayoweza kutumika kumtuhumu mtoto kama huyo kuwa ni adui wa Israel au kuhalalisha mashambulizi ya aina hii.” Kauli hii ya kushtua ya Jaji Srinivasan Muralidhar —mwenyekiti wa Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu—inajumuisha mashtaka yaliyotolewa dhidi ya utawala wa Kizayuni katika ripoti ya hivi karibuni zaidi ya kamisheni hiyo. Ripoti ambayo ikiwa matokeo yake, yatawasilishwa mbele ya vyombo vya mahakama vya kimataifa, yatafanya dunia kukabiliwa na moja ya vipindi vyenye giza kubwa zaidi katika historia ya sasa.

Hapa, si wanajeshi bali ni watoto wachanga na wenye umri mdogo ndio wamekuwa “walengwa maalumu” wa vita. Ripoti ya kikao cha 62 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa—yenye kichwa cha habari cha kutia wasiwasi kinachosomeka “Umbo la Utotoni Laharibiwa”—ni matokeo ya miezi kadhaa ya uchunguzi wa maelfu ya hati, picha za setilaiti, ripoti za uchunguzi wa kimatibabu, na ushuhuda kutoka kwa madaktari, wafanyakazi wa misaada, na mashuhuda, pamoja na video zilizotolewa na baadhi ya wanajeshi wa Kizayuni.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba kati ya Oktoba 2023 na Oktoba 2025, watoto wasiopungua 20,000 wa Kipalestina walipoteza maisha na makumi ya maelfu zaidi walijeruhiwa. Takwimu hizi pekee zinafichua kuwa watoto wamekuwa wahanga wakuu wa hujuma za Wazayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Hata hivyo, kinachotofautisha ripoti hii na nyingine za awali ni sisitizo lake juu ya umakusudi uliofanyika na si makosa ya kijeshi. Akitoa ushahidi wa kimatibabu, Muralidhar anasema kwamba idadi kubwa ya watoto waliuawa kwa kupigwa risasi kichwani na shingoni—majeraha ambayo, kulingana na wataalamu wa upelelezi, yalikusudiwa kusababisha madhara makubwa zaidi. Mbali na hayo, matumizi ya quadcopter zilizo na kamera za joto—zinazoweza kutofautisha kati ya watoto na watu wazima— zinafutilia mbali madai yoyote kwamba waathiriwa walilengwa kimakosa. Cha kushangaza zaidi ni kwamba baadhi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni, katika mahojiano na vyombo vya habari, wameelezea kulengwa watu maalum kupitia ndege zisizo na rubani kwa kutumia lugha inayofanana na “mchezo wa video.” Zaidi ya yote, simulizi hii inabainisha wazi kukiukwa mipaka ya maadili katika uwanja wa vita.

Katika sheria za kimataifa, kanuni ya kutofautisha kati ya wapiganaji na raia wa kawaida ni nguzo muhimu zaidi katika kulinda wanadamu wakati wa vita. Watoto, wanawake, wagonjwa, hospitali, shule, na vituo vya malezi ya watoto lazima vilindwe dhidi ya aina yoyote ya mashambulizi. Hata hivyo, hali inayoendelea Gaza kwa sasa inatoa picha tofauti kabisa. Uharibifu mkubwa wa shule, mashambulizi ya makusudi dhidi ya hospitali, uharibifu wa vituo vya matibabu, kulengwa kambi za wakimbizi wa ndani, na kunyimwa chakula, maji, dawa na vifaa vya matibabu idadi kubwa ya watu katika ukanda huo kunaibua swali muhimu katika uwanja huo: Je, ikiwa hakutakuwa na mahali salama kwa raia, madai ya kulindwa wanadamu yatakuwa na maana gani?

Katika ripoti yake, Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imekwenda mbali zaidi ya kurekodi takwimu za majeruhi ili kuangazia jambo muhimu: Kulengwa watoto, akina mama wajawazito, vituo vya matibabu, na miundombinu ya afya si kulengwa kizazi cha sasa tu bali ni kushambuliwa mustakabali wa taifa.

Muralidhar anasisitiza kuwa kulindwa watoto wa Kipalestina kunafungamana moja kwa moja na haki ya watu wa Palestina ya kujitawala, na kwamba kushambuliwa watoto ni kushambuliwa uhai wa jamii nzima ya baadaye. Ni kwa kuzingatia ukweli huu ndipo wataalamu wengi wa sheria za kimataifa wakaviita vitendo vya kikatili vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina kuwa mauaji ya kimbari.

Kuhusu hili, tabia ya jamii ya kimataifa pia imekuwa sehemu ya mgogoro huu. Licha ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuchukua hatua kadhaa za kidhahiri kwa madai ya kulinda watu wa Gaza; lakini kwa mujibu wa mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi, hakuna hata moja kati ya hatua hizi iliyofanikiwa kusimamisha jinai zinazoendelea za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Zaidi ya yote, hali hii inafichua udhaifu mkubwa wa mfumo wa kimataifa katika kutekeleza sheria, mfumo ambao utekelezaji wa maamuzi hautegemei sana sheria yenyewe, bali utashi wa kisiasa wa mataifa makubwa. Mataifa yaleyale ambayo katika baadhi ya sehemu huwa mepesi kutetea haki za watoto, utu wa binadamu, na kuzungumzia umuhimu wa kuadhibiwa wahalifu wa vita, lakini katika migogoro mingine ya kimataifa, kama maangamizi ya kizazi ya Gaza huonyesha undumakuwili wa wazi, kwa kukaa kimya mbele ya jinai za kila siku dhidi ya watoto, wanawake, wazee na miundombinu iliyoharibiwa kwa makusudi. Ubaguzi huu sio tu umeanika peupe madai ya uongo ya nchi hizo kuhusu kuheshimu haki za binadamu bali pia umeondoa imani ya umma kwa taasisi muhimu zinazopaswa kulinda sheria kimataifa. Nukta ya kushtua zaidi katika ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa si takwimu za wahanga, bali ni lugha iliyotumika katika utangulizi wake: “Watoto wachanga walilengwa kwa makusudi na kwa namna maalum.” Ikiwa dunia itaendelea kukaa kimya na kuonyesha undumakuwili kuhusu suala hili, wahanga hawatakuwa watoto wa Palestina pekee, bali sheria za kimataifa, dhamiri ya mwanadamu, na maadili pia vitakuwa wahanga wakuu wa sera za kinafiki za nchi za Magharibi zinazodai kutetea utu na masuala ya kibinadamu duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *