
Katika hali ya sasa ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, suala la Lebanon limeibuka kama moja ya mihimili mikuu na muhimu katika mazungumzo ya kidiplomasia na vyombo vya habari. Katika uwanja huu, sisitizo la Iran la kusitishwa kikamilifu uvamizi wa utawala haramu wa Israel nchini Lebanon kama sharti la mazungumzo na Washington limeibua maswali mengi miongoni mwa wachambuzi wa kikanda na kimataifa. Msimamo huu sio hitajio la kimkakati tu bali ni sehemu ya mantiki pana ya kimkakati ya sera za kigeni
Kifungu kunachozungumzia udharura wa kusitishwa kikamilifu uchokozi wa Israel huko Lebanon katika mazungumzo ya Iran na Marekani, kinaonyesha kwamba, kwa mtazamo wa Iran, mafaili ya usalama wa kikanda hayawezi kutenganishwa na mchakato mzima wa mazungumzo ya pande mbili hizi.
Katika miaka ya karibuni, Lebanon imekuwa moja ya sehemu nyeti zaidi za mzozo usio wa moja kwa moja kati ya Iran na Marekani na washirika wao wa kikanda. Hali ya kijiopolitiki ya nchi hiyo, uwepo wa wahusika wengi wa ndani na nje, na nafasi ya makundi ya muqawama katika milinganyo ya usalama inamaanisha kwamba mvutano wowote nchini Lebanon unaathiri moja kwa moja wachezaji wengine wa kikanda. Kwa mtazamo wa Iran, mwendelezo wa mvutano au migogoro nchini Lebanon si suala la ndani tu, bali ni sehemu ya mnyororo mrefu wa mvurugiko wa utulivu katika eneo zima la Mashariki ya Kati ambao unaweza kufunika mchakato wowote wa kidiplomasia. Kwa hivyo, Tehran inaamini kuwa hakuna amani ya kudumu inayoweza kupatika katika eneo bila kusimamishwa kabisa mapigano huko Lebanon. Kwa mtazamo wa Tehran, ikiwa mazungumzo yataendelea katika ngazi ya kisiasa pekee bila kuzingatia hali ya uwanja mpana wa vita, uwezekano wa kutokea tena mgogoro katika hatua zinazofuata ni mkubwa. Iran inasisitiza kwamba makubaliano yoyote ya kisiasa bila kuwepo dhamana ya utekelezaji ardhini yataahirisha tu mgogoro uliopo badala ya kuutatua kabisa. Hii ndio maana suala la kusitishwa mapigano nchini Lebanon likawasilishwa kama sharti la msingi la kuendelea na mazungumzo na Marekani.
Msimamo wa Iran kuhusu suala hili unaweza kuchanganuliwa kwa mitazamo kadhaa:
Kwanza, katika ngazi ya usalama wa taifa: Iran inaamini kwamba kuendelea kwa mvutano nchini Lebanon kunaweza kueneza machafuko na ukosefu wa usalama katika mhimili mzima wa muqawama na hivyo kuathiri usalama wake wa taifa.
Pili, katika ngazi ya mazungumzo ya kimataifa: Tehran inashikilia kwamba makubaliano yoyote na Marekani yatakuwa na maana tu pale yatakapoweza kupunguza mvutano katika eneo zima.
Tatu, katika ngazi ya kuzuia hujuma: Kwa mtazamo wa Iran, kufungamanisha mazungumzo ya kidiplomasia na hali ya vita uwanjani ni mbinu ya kuzuia vitendo vya uchokozi vinavyoweza kufanywa na upande wa pili wa adui.
Kwa ujumla, sisitizo la Iran la kusimamishwa mapigano kikamilifu nchini Lebanon kama sharti la kuendelea na mazungumzo na Marekani linapaswa kuchanganuliwa ndani ya mfumo mzima wa usalama wa kikanda, ambao unasema kwamba hakuna makubaliano endelevu yanayoweza kupatikana bila kuambatanishwa mazungumzo ya kisiasa na harakati za kijeshi katika uwanja wa vita kwa wakati mmoja. Kwa mtazamo huu Lebanon si suala tofauti bali ni sehemu ya upeo mpana wa usalama wa kikanda, ambao pia unaunda mustakabali wa mazungumzo ya Iran na Marekani. Wakati huo huo, msimamo huu wa Iran una ujumbe muhimu wa kimkakati: Kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika mazungumzo yake ya kikanda na kimataifa, haipuuzi usalama na maslahi ya washirika wake. Kwa sababu hii, makubaliano yoyote yanayokusudiwa kuunda utaratibu mpya katika eneo lazima, kwa mtazamo wa Iran, yazingatie pia maslahi na usalama wa wahusika wote walio na misimamo inayofanana.
Fikra ya “Umoja wa Medani” pia ina umuhimu maalum hapa. Fikra hii, ambayo imekuwa na taathira kubwa kikanda katika miaka ya karibuni, imesimama juu ya msingi kwamba tukio lolote la usalama linalotokea katika upande mmoja wa mrengo wa muqawama lina taathira za moja kwa moja katika pande nyingine za mrengo huo, na hivyo hatima zao haziwezi kutenganishwa. Kwa mtazamo wa Tehran, Lebanon, Palestina, Iraq na maeneo mengine ya muqawama ni sehemu ya mfumo mmoja wa usalama uliounganishwa, na kwamba utulivu wa kudumu utaweza kudhaminiwa tu pale medani hizi zote zitakaposhughulikiwa kwa usawa kwa wakati mmoja.
Msimamo huu, kwa kweli, unaonyesha mkakati mkubwa unaouchukulia usalama wa kikanda kama usiogawanyika na unashikilia kwamba hakuna makubaliano endelevu yanayoweza kufikiwa bila kuzingatia hali halisi ya nyanjani, maslahi ya washirika na kanuni ya ‘Umoja wa Medani’.