DAR ES SALAAM: Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limesema Tozo ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bandari (PID Levy) iliyoanza kutekelezwa Julai 1, 2026, itasaidia kuimarisha sekta ya viwanda, kuboresha miundombinu ya bandari na kuongeza ushindani wa biashara nchini.
Katika taarifa yake kwa umma, TPSF imeeleza kuwa mfumo wa tozo hiyo umeandaliwa kwa ushirikiano na Serikali ili kuhakikisha unaweka uwiano kati ya uwekezaji katika miundombinu ya bandari na kulinda mazingira bora ya biashara kwa sekta binafsi.
Kwa mujibu wa shirikisho hilo, mizigo inayolipa ushuru wa forodha itatozwa PID Levy ya asilimia 4.5 ya ushuru huo, huku malighafi za viwandani na mizigo iliyosamehewa ushuru zikitozwa asilimia 1.5 pekee ili kupunguza gharama za uzalishaji na kulinda ushindani wa viwanda vya ndani.
TPSF imeongeza kuwa mizigo ya kimiminika kwa wingi (Liquid Bulk Cargo) haitatozwa tozo hiyo, huku bidhaa nyingine za uagizaji wa ndani zikiendelea kutozwa kwa viwango vilivyowekwa.
–
Shirikisho hilo linasema utofauti wa viwango hivyo umewekwa mahsusi kulinda shughuli za uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuhamasisha uwekezaji mpya katika sekta ya viwanda.
–
Aidha, TPSF imebainisha kuwa mapato yatakayokusanywa kupitia PID Levy yatawezesha upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya bandari, kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo, kupunguza msongamano na kufupisha muda wa utoaji wa huduma.
Kwa mujibu wa TPSF, hatua hizo zitasaidia kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi katika mnyororo wa ugavi na kuifanya Tanzania kuwa kitovu chenye ushindani zaidi wa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Shirikisho hilo limewahimiza wadau wa sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa PID Levy, likisema uwekezaji wa sasa katika miundombinu ya bandari utachangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya sekta ya viwanda kwa muda mrefu.
