Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa (WMO) limetangaza kuwa hali ya mkondo joto baharini au El Niño imeanza katika ukanda wa kitropiki wa bahari ya Pasifiki na inatarajiwa kuimarika kwa kasi kati ya mwezi huu wa Julai na Septemba 2026. 

Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi siku ya Ijumaa, mwanasayansi wa shirika hilo Alvaro Silva amesema “hali hiyo itaongeza uwezekano wa mawimbi ya joto, ukame, mvua kubwa na matukio mengine ya hali mbaya ya hewa katika maeneo mengi duniani.”

Madhara kwa Afrika

Kwa mujibu wa WMO, athari mbayá za El Niño barani Afrika zitatofautiana kulingana na eneo. 

Nchi zinazopakana na Ghuba ya Guinea zinatarajiwa kupata mvua nyingi kuliko kawaida, wakati Ukanda wa Pembe ya Afrika unakabiliwa na uwezekano mkubwa wa mvua chache na ukame, hali inayoweza kuhatarisha uzalishaji wa chakula, upatikanaji wa maji na vyanzo vya kujipatia kipato kwa mamilioni ya watu.

Wito wa kujiandaa mapema

WMO imezitaka serikali, mashirika ya kibinadamu na sekta nyeti zinazoathiriwa vibaya na mabadiliko ya tabianchi, kama kilimo na afya kutumia utabiri wa hali ya hewa na mifumo ya tahadhari za mapema ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kujitokeza.

 Shirika hilo linasema hatua za maandalizi zinaweza kuokoa maisha, kulinda uchumi na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na majanga yanayoweza kusababishwa na El Niño.

Soma taarifa nzima hapa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *