Dar es Salaam. Staa wa Bongofleva, Alikiba anaendelea kuzichanga vizuri karata zake dhidi ya mshindani wake mkubwa kimuziki nchini ambaye ni Diamond Platnumz, mwanzilishi wa lebo ya WCB Wasafi.
Alikiba, mshindi wa tuzo ya MTV EMAs 2016, ameendelea kushirikiana kikazi na waliokuwa watu wa karibu wa Diamond, jambo ambalo linazidi kukuza ushindani wao.
Mvutano kati ya wawili hao umekuwapo kwa miaka mingi, kwa mara ya kwanza ulionekana baada ya Alikiba kuachia wimbo wake, Mwana (2014) kufuatia kupumzika muziki kwa miaka zaidi ya miwili.
Wakati huo Alikiba alijitambulisha kama Mfalme wa Bongofleva aliyerejea kukalia kiti chake, kauli ilipigwa na mashabiki wengi wa Diamond ambaye alikuwa akifanya vizuri, na tangu wakati huo wawili hao ni washindani kweli kweli.
Alikiba, mwanzilishi wa lebo ya Kings Music, miaka ya hivi karibuni ameonekana kushirikiana na wasanii ambao wameondoka kwenye lebo ya Diamond ya WCB Wasafi, hatua ambayo imekosolewa na kuungwa mkono na baadhi ya mashabiki.
Wanaokosoa wanasema kwanini Alikiba anataka kuendelea kuwepo kwenye muziki kupitia wasanii waliotengenezwa na mshindani wake, na wanaomuunga mkono hoja yao ni kwamba hiyo ndio njia sahihi ya kuendeleza ushindani.
Jambo hilo linazidi kuwa na maoni mchanganyiko kwa sababu wasanii hao wengi wao hawana tena maelewano mazuri ya kikazi na Diamond, hivyo huwenda Alikiba ameona hiyo ni kete muhimu dhidi ya mshindani wake huyo.
Hadi sasa wasanii walioachana na WCB Wasafi yake Diamond, na kisha kuja kushirikiana na Alikiba ni Rayvanny, Mbosso na Harmonize, mwanzilishi wa lebo ya Konde Music Worldwide.
Rayvanny katika albamu yake ya pili, The Big One (2024) yenye nyimbo 18 huku akisimamiwa na Next Level Music (NLM), Alikiba alisikika katika wimbo namba tatu uitwao Naoa.
Hii ndio ilikuwa mara ya kwanza kwa Alikiba kufanya kazi na aliyekuwa mwanamuziki wa WCB Wasafi. Kolabo hiyo ilifanya vizuri kwa kiasi chake, na hadi video yake ikiwa imetazamwa (views) YouTube zaidi ya mara milioni 7.3.
Utakumbuka Rayvanny alitoka rasmi kimuziki chini ya WCB Wasafi kupitia wimbo wake, Kwetu (2016), na alikuja kuachana na lebo hiyo mnamo Julai 2022 baada ya kuanzisha yake ya NLM.
Tukija kwa Mbosso, hapa ndipo Alikiba amechanga karata zake vizuri, kwani wakati huu ambao Mbosso anafanya vizuri ndipo amepiga naye kolabo, Bhuju (2026) ambayo inafanya vizuri kwa sasa.
Huu ndio wimbo wa kwanza kwa Alikiba kumshirikisha mwanamuziki aliyepita WCB Wasafi, lebo ambayo ilianza kuwatoa wasanii miaka 10 iliyopita ambapo Harmonize ndiye alikuwa wa kwanza.
Mbosso alitambulishwa rasmi WCB mwaka 2018 ikiwa ni takribani mwaka mmoja na nusu tangu kusambaratika kwa kundi la Yamoto Band ambalo alitamba nalo tangu mwaka 2013.
Na kwa sasa Alikiba anatamba na wimbo wake mpya, Utanionea (2026) akimshirikisha Harmonize, ni kolabo ambayo imezungumziwa tangu mwaka uliopita na mashabiki walikuwa na shauku kubwa ya kuisikia.
Shauku hiyo imetoka hasa na kile kilichotokea kati ya Harmonize na Diamond baada ya mwanamuziki huyo kuachana na WCB mwaka 2019. Mgogoro mkubwa wa kimkataba kati yao, ni moja ya mambo yaliyopelekea wawili hao kutoiva changu kimoja hadi sasa.
Hivyo, kolabo hiyo na Harmonize, mbali na biashara ya muziki iliyopo katikati yake, ilikuwa kete muhimu kwake Alikiba katika uwanja wa ushindani dhidi yake na Diamond.
Hata hivyo, kabla ya Alikiba kuanza kutamba na wasanii wa Diamond, alifanya hivyo kwa wazazi wenza wa mwanamuziki huyo ambao ni Hamisa Mobetto na Tanasha Donna kutokea nchini Kenya.
Hamisa, Miss XXL After School Bash 2010, alitokea kama video vixen katika video ya wimbo wake Alikiba, Dodo (2020) ambayo ilishutiwa Zanzibar chini ya kampuni ya Rockshot.
Naye Tanasha alishirikishwa na aliyekuwa msanii wa lebo ya Alikiba, Kings Music, Tommy Flavour katika wimbo wake, Numero Uno (2022). Kipindi cha kutayarisha video ya wimbo huo huko Zanzibar, Alikiba na Tanasha walioonekana pamoja.
Hatua hiyo ilikuja takribani mwaka mmoja baada ya Tanasha kuhudhuria uzinduzi wa pili (listening party) wa albamu ya tatu ya Alikiba, Only One King (2021) uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Tanasha ambaye kabla ya uhusiano na Diamond alionekana katika video ya wimbo wa Alikiba, Nagharamia (2015), alipanda jukwaani na kumpongeza Alikiba kwa albamu hiyo nzuri iliyokuja kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA).