MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka rekodi mpya katika ukusanyaji wa mapato baada ya kukusanya jumla ya Shilingi trilioni 37.96 katika mwaka wa fedha 2025/26, sawa na asilimia 105.24 ya lengo la kukusanya Shilingi trilioni 36.07.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, tarehe 04.07.2026 imeeleza kuwa mafanikio hayo katika makusanyo ya kodi ni sawa na ukuaji wa asilimia 17.61 ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi trilioni 32.27 yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2024/25.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kuendelea kutumia mbinu za kisasa katika usimamizi wa kodi, kuimarisha uzingatiaji wa sheria za kodi pamoja na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika miezi yote 12 ya mwaka wa fedha uliomalizika Juni 2026, TRA ilifanikiwa kuvuka malengo ya makusanyo ambapo kwa Mwezi Juni wameweka rekodi mpya kwa kukusanya Shilingi trilioni 4.01, sawa na ufanisi wa asilimia 107.98, huku Januari, Machi na Aprili pia zikifanya vizuri kwa kuvuka malengo yaliyowekwa.
Katika taarifa hiyo, TRA imeeleza kuwa mafanikio hayo yameiwezesha mamlaka hiyo kuweka rekodi mpya nne katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali nchini, hatua inayodhihirisha kuendelea kuimarika kwa mifumo ya kodi na usimamizi wa mapato.
Mamlaka hiyo imewahakikishia wananchi na wadau mbalimbali kuwa itaendelea kuboresha huduma kwa walipakodi, kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuhakikisha mapato ya Serikali yanaongezeka kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii.
Mafanikio ya TRA yanatarajiwa kuongeza uwezo wa Serikali kutekeleza bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 kupitia mapato ya ndani, sambamba na kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo ya nje.

(Feed generated with FetchRSS)