
Simba imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya leo Jumamosi, Julai 4, 2026 kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC katika Uwanja wa Gombani, Pemba.
Bao pekee lililoipa Simba taji katika mchezo huo lilipachikwa katika dakika ya 62, likiwa la kujifunga la Yahya Zayd wa Azam FC aliyeukwamisha wavuni wakati akiwa katika harakati za kuokoa mpira wa adhabu uliopigwa na Elie Mpanzu.
Simba wamepata adhabu hiyo baada ya Pascal Msindo kumuangusha Libasse Gueye nje kidogo ya eneo la hatari la Azam FC.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, Azam FC ilionekana kuamka na kujaribu kusaka bao la kusawazisha lakini safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa imara kuondoa hatari ilizoelekezewa.
Katika dakika ya 67, Azam FC ilipata pigo baada ya kiungo wake Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuonyeshwa kadi nyekundu na refa Sifu Amon.
Fei Toto alionyeshwa kadi hiyo nyekundu baada ya kumpiga ngumi Libasse Gueye ambaye alikuwa akijaribu kumdhibiti wakati alipokuwa na mpira.
Kwa kutwaa taji hilo, Simba imemaliza ukame wa miaka mitano ambao ilikuwa nao kwa kukaa bila kutwaa taji hilo.
Kabla ya leo, Simba ilitwaa ubingwa huo Julai 25, 2021 kwa kuifunga Yanga kwa bao 1-0 katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Simba imeendeleza pia rekodi yake nzuri ya kutopoteza mechi ya fainali ya mashindano hayo ambapo tangu yaliporudi kwa mara ya kwanza msimu wa 2015/2016, imecheza mechi nne za hatua ya fainali na imeshinda zote.
Kichapo cha leo kimeendeleza nuksi ya Azam FC kupoteza mechi za fainali katika msimu huu ambapo kabla ya fainali ya jana, ilifungwa pia katika fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu.
Simba pia imelipiza kisasi cha kupoteza mechi ya nusu fainali ya mashindano hayo dhidi ya Azam FC, msimu wa 2022/2023 ilipochapwa mabao 2-1.