Arusha. Kutowasilishwa mahakamani kwa picha mjongeo (video) iliyodaiwa kuwaonyesha washambuliaji, kuchelewa kwa shahidi mkuu kuwataja watuhumiwa na ushahidi uliobainika kuwa wa uvumi, kumewaepusha watu watatu adhabu ya kunyongwa baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kubaini upande wa mashtaka haukuthibitisha bila shaka kuwa wao ndio waliomuua Dickson Kamenya.

Walionusurika adhabu hiyo ni Barnabas Andrea (fundi seremala katika Taasisi ya Afya Kabanga), Lameck John na Ibrahim Kileha, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Chekenya.

Hukumu hiyo imetolewa Julai 3, 2026, Jaji Augustine Rwizile, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Msingi wa kesi

Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na shtaka la mauaji kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, wakidaiwa kumuua Dickson Oktoba 19, 2023 katika eneo la Sinza, Wilaya ya Kasulu, Mkoa wa Kigoma.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, siku ya tukio washtakiwa walimwomba Tumaini Festo awaonyeshe alikokuwa marehemu kwa madai kwamba walikuwa na kazi ya uashi kwa ajili yake.

Baada ya kufika nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza, ilidaiwa kuwa Dickson (marehemu) na Tumaini walituhumiwa kuiba mali ambayo haikutajwa, kisha wakafungwa kwa kamba na kushambuliwa kwa fimbo, nyaya za umeme na mateke.

Mashtaka yalidai kuwa wawili hao baadaye walipelekwa katika Mto Bogwe ambako waliendelea kupigwa na kuloweshwa majini kabla ya kuachwa wakiwa katika hali mbaya.

Dickson alikutwa siku iliyofuata akiwa hana fahamu na kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kasulu kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni, ambako alifariki dunia Novemba 1, 2023.

Ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu ilionyesha kuwa chanzo cha kifo kilikuwa jeraha kubwa la ubongo lililotokana na kipigo.

Katika utetezi wake, mshtakiwa wa kwanza aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio alikuwa kazini akitengeneza madawati ya wanafunzi na kuwa aliingia tangu saa moja asubuhi na kuondoka saa tatu na nusu usiku, hivyo hakuwepo eneo la tukio.

Ili kuunga mkono utetezi wake, aliwasilisha kitambulisho chake cha kazi na rejista ya mahudhurio, huku Ofisa Rasilimali Watu wa Taasisi ya Afya ya Kabanga akithibitisha kuwa alikuwepo kazini siku hiyo.

Pia alikana kuwa marehemu alishambuliwa nyumbani kwake kama ilivyodaiwa na upande wa mashtaka.

Kwa upande wake, mshtakiwa wa pili alikana kuhusika na mauaji hayo akidai kuwa Oktoba 19, 2023 alikuwa akifanya kazi katika shamba la dada yake lililopo Kijiji cha Nyachenda kuanzia asubuhi hadi saa 11 jioni, akiwa pamoja na dada yake, shemeji yake na wafanyakazi wawili.

Aliiambia mahakama hakumjua marehemu wala kushiriki kwa namna yoyote katika tukio hilo.

Mshtakiwa wa tatu, Ibrahim, ambaye ni mwalimu, alidai kuwa siku ya tukio alifika shuleni saa moja na dakika nane, akafundisha siku nzima na hakuwahi kuondoka katika eneo la kazi.

Aliwasilisha rejista ya mahudhurio ya shule pamoja na kitambulisho chake cha kazi kuthibitisha utetezi wake. Mwalimu mwenzake, Anderson Yakobo, alieleza mahakama kuwa waliripoti kazini pamoja, wakasaini rejista ya mahudhurio na kubaki shuleni katika muda wote wa kazi siku hiyo.

Uamuzi Mahakama

Jaji Rwizile amesema pamoja na upande wa mashtaka kuthibitisha kuwa Dickson alifariki kutokana na kipigo kikali kilichomsababishia jeraha kubwa la ubongo, haukuweza kuthibitisha bila shaka yoyote kuwa washtakiwa hao ndio waliohusika na shambulio lililosababisha kifo hicho.

Jaji amesema shahidi mkuu wa upande wa mashtaka, ambaye alidai kushuhudia tukio lote, hakuwataja mara moja washtakiwa kwa ndugu zake wala kwa polisi baada ya kupata fahamu, licha ya kudai kuwa alikuwa akiwafahamu kabla ya tukio.

Mahakama ilieleza kuwa hata katika taarifa yake ya polisi, shahidi huyo hakuyataja majina ya washtakiwa, jambo lililoibua mashaka makubwa kuhusu uaminifu wa utambuzi wake wa baadaye.

Aidha, mahakama ilibaini kuwa ushahidi wa mashahidi wa mashtaka ulikuwa na tofauti kuhusu namna washtakiwa walivyotambuliwa.

Amesema shahidi mmoja wa Jamhuri alidai kuwaona wakitekeleza shambulio hilo, huku mashahidi wengine wakieleza kuwa waliwatambua kupitia video iliyodaiwa kurekodiwa na mtu ambaye hakufikishwa mahakamani kutoa ushahidi.

Jaji huyo amesema video hiyo haikuwasilishwa mahakamani kama kielelezo, huku kifaa kilichotumika kuirekodi kikidaiwa kutopatikana, hivyo maelezo yaliyotolewa kuhusu video hiyo yalibaki kuwa ushahidi wa uvumi usioweza kuthibitisha hatia ya washtakiwa.

Mahakama pia iliona kulikuwa na utofauti wa maelezo kuhusu mazingira ya tukio, ikiwemo maelezo ya eneo la nyumba ambako shambulio lilidaiwa kuanzia, hali iliyoendelea kudhoofisha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Kutokana na dosari hizo, mahakama imesema tuhuma dhidi ya washtakiwa zilibaki katika kiwango cha mashaka na hazikufikia kiwango cha kuthibitisha kosa la jinai bila shaka yoyote, kama sheria inavyotaka.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama iliwakuta washtakiwa wote watatu hawana hatia na kuamuru waachiwe huru mara moja isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *