Dar es Salaam. Tanzania na Angola zimedhamiria kugeuza uhusiano wake kutoka wa kidiplomasia kuwa wa kiuchumi kwa kuongeza uwekezaji, biashara na ushirikiano wa viwanda, huku zikilenga kufungua fursa mpya za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili.

Dhamira hiyo ilibainishwa jana Julai 4,2026 wakati wa kongamano la Siku ya Angola lililofanyika katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba.

Kupitia kongamano hilo, Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalumu za Kiuchumi Tanzania (Tiseza) iliwasilisha fursa za uwekezaji zilizopo katika Kanda Maalumu za Kiuchumi (SEZ) na Maeneo ya Uzalishaji kwa Ajili ya Mauzo ya Nje (EPZ),  ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuvutia wawekezaji kutoka Angola na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Akizungumza katika kongamano hilo, Balozi wa Angola nchini Tanzania, Domingos De Almeida Da Silva Coelho alisema Tanzania na Angola zina historia ndefu ya uhusiano wa kirafiki, lakini kipaumbele cha sasa ni kuhakikisha uhusiano huo unazaa matokeo halisi ya kiuchumi kupitia uwekezaji na biashara.

“Angola na Tanzania zina urafiki wa muda mrefu, lakini kipaumbele sasa ni kuugeuza urafiki huo kuwa ushirikiano wa vitendo katika uwekezaji na biashara ambao utazalisha ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisema.

Alisema majukwaa ya kimataifa kama maonyesho ya Sabasaba yana nafasi muhimu katika kuwaunganisha wawekezaji, wafanyabiashara na taasisi kutoka nchi mbalimbali, hivyo kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji.

“Haya si maonyesho ya bidhaa pekee, bali ni fursa ya kujenga madaraja ya kudumu ya kiuchumi kati ya mataifa yetu,” alisema.

Katika kongamano hilo, Tiseza iliwasilisha maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali katika mazingira ya uwekezaji, ikieleza kuwa hatua hizo zinalenga kurahisisha taratibu za uwekezaji na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) katika sekta mbalimbali za kipaumbele.

Ofisa Mwandamizi wa Uwekezaji wa TISEZA, Vedasto Kagombora alisema Serikali imeendelea kuimarisha sera na mfumo wa udhibiti wa uwekezaji ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na mazingira thabiti, yanayotabirika na yenye ushindani kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Alisema SEZ na EPZ zinaendelea kuwa nguzo muhimu katika ajenda ya Serikali ya kuharakisha maendeleo ya viwanda hususan katika kukuza sekta ya uzalishaji, kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kuimarisha uongezaji thamani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Maeneo haya ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya viwanda, kuongeza mauzo ya nje na kuzalisha ajira zenye tija, hususan kwa vijana,” alisema.

Ili kufanikisha hilo, Serikali inaendelea kutekeleza maboresho yanayolenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wawekezaji na kupunguza vikwazo vya kiutawala vinavyoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji.

“Tumejizatiti kuhakikisha wawekezaji wanaochagua Tanzania wanapata huduma kwa ufanisi, uwazi na ushindani,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *