Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump amesema alikuwa akifuatilia mazishi ya kiongozi wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, na kushangazwa na kuona baadhi ya Wairani wakilia wakati wa mazishi.
Akizungumza na tovuti ya habari ya Axios, Trump alisema alikuwa na dhana kwamba watu wengi nchini Iran walimchukia Ali Khamenei.
Hata hivyo, baada ya kutafakari kwa muda, alinukuliwa akisema: “Huenda machozi hayo si ya kweli.”
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Trump alirudia madai yake kwamba Wairani walikuwa “wakisihi kufikiwa kwa makubaliano”.
Aidha, alisema pande zote mbili zimekubaliana kusitisha mazungumzo kwa muda wa wiki moja hadi shughuli za mazishi zitakapokamilika.
Trump aliongeza kuwa katika kipindi hicho, hakuna upande utakaofyatulia mwenzake risasi. Alisema: “Wote wako hapo. Risasi moja tu ingeweza kuwaondoa wote, lakini hatutafanya hivyo, kwa sababu hapo hatutakuwa na mtu wa kufanya naye mazungumzo.”
Rais huyo wa Marekani pia aliiambia Axios kwamba Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameomba kukutana naye katika Ikulu ya White House, na kwamba mkutano huo unaweza kufanyika baada ya kurejea kutoka mkutano wa NATO wiki ijayo.
Akizungumzia uhusiano wake na Netanyahu, Trump alisema: “Tuna uhusiano mzuri sana. Anajua nani mwenye mamlaka.”
Axios ilieleza kuwa huo utakuwa mkutano wao wa kwanza tangu Februari, wakati Benjamin Netanyahu alipowasilisha mpango wake wa vita dhidi ya Iran.
Tangu wakati huo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wa karibu na Trump wamekuwa wakizidi kukata tamaa kuhusu Netanyahu.
Afisa mmoja wa Marekani alinukuliwa akisema: “Washauri wengi wa karibu wa Trump wanaamini kwamba Benjamin Netanyahu alikuwa na makosa kuhusu kila jambo.”
Soma zaidi: