
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mashambulizi dhidi ya nchi kadhaa za eneo la Asia Magharibi na umekuwa chanzo cha migogoro mingi pamoja na hali ya ukosefu wa usalama, huku akibainisha kwamba, nchi za Kiislamu hazijawahi kuanzisha mashambulizi ya aina hiyo.
Rais Pezeshkian aliyasema hayo Jumamosi jioni aliposhiriki katika Kongamano la Kimataifa la “Imam Khamenei; Kiongozi wa Milele wa Muqawama“, ambapo alianza kwa kutoa heshima kwa mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini, pamoja na kiongozi shahidi wa Mapinduzi na mashahidi wote waliotoa maisha yao kwa ajili ya kulinda uhuru, heshima na utukufu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Aidha, Rais Pezeshkian aliwashukuru wageni na washiriki wote wa kongamano hilo waliotoka ndani na nje ya Iran kwa kushiriki katika tukio hilo muhimu.
Rais wa Iran pia aligusia ushiriki mkubwa wa viongozi na wageni kutoka sehemu mbalimbali za dunia katika shughuli za kutoa heshima za mwisho na mazishi ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, akieleza matumaini yake kwamba, ushiriki huo utachangia kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu. Aidha, alisisitiza kuwa mataifa ya Kiislamu yanapaswa kusimama kwa mshikamano mkubwa zaidi katika kukabiliana na sera za mauaji ya kulenga watu, matumizi ya nguvu na umwagaji damu zinazotekelezwa na madola yenye nguvu.
Pezeshkian pia alisisitiza nafasi ya kipekee aliyokuwa nayo Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akisema kuwa, ukubwa wa hadhi yake, haiba yake, uwezo wake wa uongozi na uthabiti wake ni vikubwa mno kiasi kwamba haviwezi kuelezwa kikamilifu kwa maneno. Aliongeza kuwa, hisia zinazoonekana leo miongoni mwa wananchi, machozi yao na mahudhurio yao makubwa katika shughuli mbalimbali ni ushahidi wa wazi wa nafasi kubwa aliyokuwa nayo kwa wananchi wa Iran na watu wote wapenda uhuru duniani.
Aidha, Rais Pezeshkian alizungumzia uhalifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa Marekani, akisema kuwa, kwa sasa eneo la Asia Magharibi linashuhudia kampeni ya mauaji ya kulenga watu mahususi, inayowalenga wasomi, wanasayansi na watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii.
Aliongeza kuwa vitendo hivyo vinafanyika kwa mbinu mbalimbali katika Ukanda wa Gaza, Lebanon, Syria, Iraq, Iran na nchi nyingine za eneo hili, akisisitiza kuwa hali hiyo imeendelea kuzidisha migogoro na kuhatarisha usalama wa eneo zima.