Amesema hay oleo huko Geneva Uswisi mwanzoni mwa mkutano wa kwanza wa Mjadala wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usimamizi wa AI unaofanyika kwa siku mbili kuanzia leo huko Geneva, Uswisi.

Katibu Mkuu amesisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha mabilioni ya watu ambao bado hawawezi kupata teknolojia hii ya mapinduzi wanapata fursa ya kuitumia.

Amesema kuwa makubaliano yoyote ya baadaye yanapaswa kuwa “yanayostahili kuaminiwa na dunia nzima,” yaweke usalama mbele, hasa usalama wa watoto, ili kuwalinda dhidi ya ulaghai na unyanyasaji unaotokana na maudhui yanayotengenezwa kidijitali.

Akisisitiza ujumbe huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, amehimiza mataifa kushirikiana kukabiliana na upande wa kutisha wa AI. Amebainisha kuwa takribani asilimia 99 ya video na picha bandia au (deepfakes) zina maudhui ya kingono, na asilimia 96 kati yake huwalenga wanawake na wasichana.

© UNICEF/Safidy Andrianantenain Wanafunzi katika shule moja huko Taolagnaro, Madagaska, wakiwa kwa mafunzo katika maabara yao mpya ya kompyuta kwa mara ya kwanza.

Kupunguza pengo la kidijitali

Katibu Mkuu amesema  kuwa miongoni mwa vipaumbele vya udhibiti wa AI ni kuhakikisha nchi zinazoendelea zinapata fursa ya kutumia teknolojia hiyo, na kwamba vituo vyote vya kuhifadhi na kuchakata data za AI vitumie nishati mbadala ifikapo mwaka 2030.

Amesema kuwa ingawa AI iko katikati ya mustakabali wa pamoja wa binadamu, ni lazima ibaki kuwa teknolojia ambayo “mashine zinaweza kutoa taarifa, lakini binadamu ndio wanaopaswa kufanya maamuzi na kuwajibika.”

Huu ni mwendelezo wa wito alioutoa kwa mara ya kwanza mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2017.

Mapinduzi ya AI

Katika miaka mitatu tangu AI ilipoanza kutumika kwa kiwango kikubwa, imeleta mabadiliko makubwa katika uchumi na jamii, kwa manufaa na pia kwa madhara. Umoja wa Mataifa umeongoza juhudi za kimataifa za kuweka mfumo wa usimamizi wa AI, ambazo zilifikia hatua muhimu kupitia mkutano huu wa kwanza wa Geneva.

Mkutano huo unakutanisha kampuni mbalimbali, watafiti, wataalamu wa teknolojia, mashirika ya kiraia, pamoja na mtunzi wa muziki wa kitamaduni aliyebadilika kuwa msanii wa sanaa za kidijitali, Gadi Sassoon, kujadili namna ya kuhakikisha AI inamtumikia binadamu. Mazungumzo ya pili yanatarajiwa kufanyika mwezi Mei 2027 mjini New York City.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Teknolojia za Kidijitali na Zinazochipuka, Amandeep Singh Gill, amesema:

“AI ina athari kubwa sana kiasi kwamba haiwezi kuachwa iundwe na wachache pekee. Tunahitaji mjadala wa kimataifa, unaojumuisha kila mtu na unaotegemea ushahidi.”

Kwa upande wake, mwenyekiti mwenza wa Jopo Huru la Kimataifa la Kisayansi kuhusu AI, Yoshua Bengio, amesema hakuna dalili kwamba kasi ya maendeleo ya AI itapungua. Ameongeza  kuwa majaribio yameonesha kuwa mifumo ya kisasa ya AI inaweza hata kuwahadaa binadamu na kutambua inapokuwa inafanyiwa majaribio.

Amesema, “inaweza kusikika kama hadithi za kisayansi, lakini hili ni jambo linalowezekana. Linaweza kubadilisha dunia kwa njia ambazo bado hatuzielewi, na kubadilisha mizani ya nguvu duniani kwa namna inayohitaji umakini wetu.”

© Adobe Stock/Pinkeyes Fundi anafanya kazi katika kituo cha huduma ya data.

Mlolongo wa maendeleo ya udhibiti wa AI

  • 2017: Katibu Mkuu António Guterres alitoa wito wa kwanza wa kuwepo kwa udhibiti wa AI, akitambua uwezo wake mkubwa lakini pia akionya kuhusu athari zake kwa ajira, usalama wa dunia na mfumo wa jamii.
  • 2023: Baraza la Ushauri la Ngazi ya Juu la Umoja wa Mataifa kuhusu AI lilipendekeza kuwepo kwa mfumo wa utawala wa AI duniani.
  • 2024: Makubaliano ya Mkataba wa Zama Zijazo (Pact for the Future) pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali, (Global Digital Compact) yalitoa msingi wa kuanzishwa kwa mfumo wa utawala wa AI.
  • Juni 2026: Jopo Huru la Kisayansi la Umoja wa Mataifa lilionya kuwa AI inaweza kusababisha madhara makubwa kutokana na matumizi mabaya au maendeleo yake yanayozidi kasi ya uelewa wa kisayansi na uwezo wa serikali kuendana nayo.
  • 6–7 Julai 2026: Mazungumzo ya kwanza ya Kimataifa kuhusu Usimamizi wa AI na Mkutano wa AI kwa Maslahi ya Wote yalifanyika Geneva.

AI kama “msawazishaji mkubwa”

Katibu Mkuu amesema kuwa ikiwa AI itatumika vizuri na kusambazwa kwa usawa, inaweza kufupisha maendeleo ya miongo kadhaa na kuyafanya ndani ya miaka michache, hivyo kuwa “msawazishaji mkubwa wa karne ya 21.”

Hata hivyo, kabla ya hapo, AI lazima ifanyiwe majaribio ya kina ya usalama na kuwe na uwajibikaji wa wazi kisheria.

Amesema, “nchi zinapokubaliana namna ya kupima mifumo, kutathmini hatari na kuwajibisha wahusika, usalama unasafiri pamoja na teknolojia. Zisipokubaliana, kutakuwa na sheria zisizolingana ambazo zitagharimu zaidi, kugawanya dunia na kutomlinda yeyote.”

Usalama wa watoto

Katibu Mkuu amependekeza mataifa yote yapitishe Ahadi ya Usalama wa Watoto katika AI, akisema, “hakuna mtoto anayepaswa kuwa majaribio ya AI isiyodhibitiwa.”

Amelinganisha hali hiyo na dawa na vifaa vya kuchezea watoto ambavyo hupimwa kwanza kabla ya kuruhusiwa kutumiwa.

Ahadi ya usalama wa watoto inataka:

  • Kampuni zihakikishe AI ni salama kwa watoto kupitia majaribio maalumu na usimamizi huru.
  • Kusiwe na uvumilivu kabisa kwa AI inayozalisha picha za kingono zinazohusisha watoto.
  • AI itambue mtoto anayeonesha dalili za msongo au hatari na kumwelekeza kwa msaada wa binadamu.
  • Hakuna kampuni inayopaswa kujitetea kwa kusema, “Mwenendo wa ufuatiliaji wa mitandao au Algoriti ndiyo ilifanya.”

Haki za binadamu

Katibu Mkuu amesema kuwa haki za binadamu hazipaswi kujadiliwa wala kupuuzwa. Amesema kwamba, “AI haipaswi kamwe kuondoa utu wa binadamu au kuimarisha ubaguzi. Katika maamuzi muhimu kama vile haki, afya na ulinzi wa sheria, mashine zinaweza kusaidia kutoa taarifa, lakini binadamu ndio wanaopaswa kufanya maamuzi na kuwajibika.”

© Adobe Stock/Kittinan Kifaa kinachosaidiwa na AI ina jukumu kubwa katika kilimo cha kisasa na utunzaji wa mimea.

Uwekezaji wa umma

Amesema uwekezaji binafsi katika miundombinu ya AI unakadiriwa kufikia dola trilioni 500, huku uwekezaji wa umma katika kujenga uwezo wa AI kwa nchi zinazoendelea ukiwa mdogo sana kwa kulinganisha.

Ili kupunguza pengo hilo, ametangaza kuwa zaidi ya nchi 20 zimeunga mkono mpango wa kuanzisha Mtandao wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa kubadilishana ujuzi na ushirikiano katika kujenga uwezo wa AI.

Ameonya, “hatuwezi kuruhusu pengo la kidijitali kubadilika kuwa pengo la AI, na pengo la AI kuwa pengo la maendeleo, usalama na hata uhuru wa mataifa.”

Wito wa uwazi

Katibu Mkuu pia amezitaka kampuni zote kubwa za AI kupima na kuweka wazi hadharani athari mbaya za mifumo yao kwa mazingira, ikiwa ni pamoja na matumizi ya hewa ya ukaa, maji na ardhi.

Amesisitiza kuwa vituo vyote vya data vinapaswa kutumia nishati mbadala ifikapo mwaka 2030. “AI inaweza kuonekana kana kwamba haina uzito wa kimwili, lakini madhara yake kwa mazingira ni halisi.”

Ameongeza kuwa vituo vya data vinatumia umeme mwingi kuliko nchi nyingi duniani, na kufikia mwaka 2030 vinaweza kutumia umeme unaozidi ule wa mataifa yote isipokuwa matano makubwa zaidi. Pia vinaweza kutumia maji ya kutosha kukidhi mahitaji ya watu bilioni 1.3 walio katika nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara kwa mwaka mzima.

Kwa sababu hiyo, Umoja wa Mataifa umeanzisha Mpango wa Uwazi wa Athari mbaya za AI kwa Mazingira ili kuhakikisha maendeleo ya AI yanakwenda sambamba na ulinzi wa mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *