Mbali na Kyiv, mashambulizi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika miji ya Sumy yameua raia kadhaa na kujeruhi makumi zaidi, wakiwemo watoto. Mikoa ya Dnipro, Kherson na Zaporizhzhia pia imekumbwa na mashambulizi yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kiraia, hali iliyokatiza upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Matthias Schmale, ambaye alitembelea maeneo yaliyoshambuliwa, amesema ni vigumu kuelezea kiwango cha mateso aliyoyashuhudia.

Ni uchungu

“Inasikitisha kushuhudia watu wakilia juu ya miili ya wanafamilia au marafiki zao, au wakingoja waokoaji waondoe vifusi ili kujua hatima ya wapendwa wao. Ni uchungu kuona kile ambacho jamii zimejenga kwa miaka mingi kikiharibiwa kwa muda mfupi,” amesema Schmale.

Amesema idadi ya raia wanaouawa na kujeruhiwa inaendelea kuongezeka, si tu katika maeneo ya mapambano bali pia katika miji, na kusisitiza kuwa sheria za kimataifa za kibinadamu zinawataka wote wanaohusika katika vita kuchukua hatua zote zinazowezekana kuwalinda raia na miundombinu ya kiraia.

“Haiwezi kurudiwa mara nyingi vya kutosha kwamba sheria za kimataifa za kibinadamu zinahitaji hatua zote zinazowezekana zichukuliwe kuwalinda raia na miundombinu ya kiraia. Mashambulizi yanayoharibu makazi ya watu na kupokonya maisha ya wasio na hatia hayapaswi kamwe kukubalika,” amesisitiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *