Ni siku nane za vijana kupaza sauti kujadili mustakabali wa amani wa taifa la Tanzania lililopo Mashariki mwa Afrika. Japokuwa midahalo hiyo imefanyika katika mikoa minne tofauti, changamoto, fursa na mapendekezo ya vijana, vyote vimejengwa juu ya msingi wa amani na usalama endelevu.

Vijana kutoka makundi mbalimbali, wakiwemo wajasiriamali, vijana wenye ulemavu, mashirika yanayoongozwa na vijana, vikundi vya kijamii na viongozi wa serikali kwa kila mkoa, wamejitokeza na kuchangia maoni yao.

Mikoa ya kusini mwa Tanzania ilifungua pazia la midahalo; Mbeya, Juni 25 na 26, kisha Songwe, Juni 27 na 28 na kufuatiwa na mikoa ya kaskazini-magharibi mwa nchi. Mwanza, Julai 2 na 3 na hatimaye mkoa wa Geita ukakunja jamvi mwishoni mwa juma liliopita Julai 4 na 5.

Nini mtazamo wa vijana? Kutoka hapa Mwanza, mmoja wa washiriki ni Vanessa Kasoga.

“Binafsi zamani nilikuwa naamini kwamba labda mafunzo haya ni kwa ajili ya watu fulani au kwa ajili ya chama fulani. Lakini safari hii nimejifunza zaidi kwamba mafunzo haya yanawagusa watu wa jamii tofauti, itikadi tofauti na makundi tofauti. Hii imenipa fursa kuona kwamba wote kwa ujumla wetu tuna nafasi ya kulijenga taifa letu lakini pia taifa letu ni kipaumbele zaidi ya mitazamo yetu ambayo tunayo katika jamii zetu. Kwa hiyo, sisi wote tuna nafasi ya kulinda na kuitunza amani lakini pia kuelimishana faida na athari ambazo zinaweza zikatupata kama tukijiingiza kwenye hali za kuondosha amani katikati yetu.”

Edmund Mbigili ni Afisa mradi wa Dumisha Amani unaofadhiliwa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Amani na Maendeleo, UNPDF, kupitia mfuko mdogo wa Amani na Usalama wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

“Tumepata mwitikio mzuri na mafunzo yalikuwa yamejikita katika maeneo mbalimbali, kwanza ni jinsi gani vijana wanaweza wakawa chachu ya kuhamasisha amani na maendeleo kwa nchi yetu, lakini ni jinsi gani vijana wanaweza kushiriki katika utatuzi wa migogoro kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya kitaifa. Na mwishowe kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa ya amani kama ilivyo siku zote.”

Frank Novatus anaeleza ni nini mtazamo wake kuhusu fursa za ajira.

“Changamoto ya kwanza ni haki sawa ya upatikanaji wa mikopo, kuwepo na uwiano sahihi wa upatikanaji wa mikopo ili kuondoa manung’uniko kwa baadhi ya vijana. Changamoto nyingine ni upatikanaji wa ajira hasa kwenye sekta binafsi na serikalini, vijana waweze kuwa na wigo mpana wa kuweza kupata ajira. Pia kwenye fursa mbalimbali ambazo vijana wanatakiwa kuzipata kuwe na uwazi kwa sababu kumekuwa na tamaduni vijana hawahusishwi kwenye maamuzi yanayowahusu, wamekuwa wakiingia wazee, na akina mama. Kwa hiyo kunapokuwa na uwajibikaji na uwazi katika mambo hayo, inaweza kukasababisha kijana asijiingize katika migogoro na uvunjifu wa amani, mwishowe tutalinda usalama wa nchi yetu.”

Vijana wenye ulemavu nao hawakubaki nyuma, James Shephard ni miongoni mwao, yeye ana ulemavu wa viungo.

“Mimi ni mnufaika mzuri sana wa haya mafunzo, hayakuwa na ubaguzi kwa sisi ambao ni walemavu. Kupitia mafunzo haya nimejifunza kuwa utunzaji wa amani na utulivu wa nchi yetu inatupasa kuanzia kwetu sisi wenyewe. Kwenye haya mafunzo tumepata njia bora zaidi za kupewa fursa mbalimbali ambazo ukijiunga unaweza ukapata mikopo na pia hiyo mikopo inaweza kutuwezesha katika biashara mbalimbali na watu kuondokana na umaskini.”

© UNDP Tanzania UNDP yaendesha midahalo ya amani na utatuzi wa migogoro kwa vijana nchini Tanzania

Kwa washiriki wa mikoa ya Songwe, Mbeya na Geita wameeleza kuwa changamoto za kijamii, kiuchumi na kisiasa zinazowakabili zinaweza kuhatarisha amani endapo hazitashughulikiwa kwa wakati na kwamba, kuwawezesha vijana katika utofauti wao si tu kunachochea maendeleo ya taifa, bali pia kunajenga jamii yenye ustahimilivu, mshikamano na usalama wa kudumu.

Sambamba na mambo mengine, midahalo hiyo pia imetoa nafasi shirikishi kwa vijana kutoa mapendekezo yatakayochangia kuandaa Mpango wa Kitaifa wa Vijana, Amani na Usalama, hatua inayoakisi dhamira ya kuhakikisha vijana wanakuwa sehemu ya kutengeneza suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii badala ya kuwa watazamaji.

Edmund Mbigili anaeleza ni nini tathmini yake.

“Mradi huu tunatekeleza kwa karibu sana kwa kushirikiana na serikali na tumekuwa na viongozi kutoka ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana,kwa hiyo kwa ujumla mawazo yao yote yanachukuliwa na wadau mbalimbali wa serikali, tumeona hata pia hapa Afisa Maendeleo ya jamii mkoa tumekuwa naye na wote kwa pamoja wanaonesha hali ya kuchukua zile changamoto za vijana na kuzifanyia kazi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *