Mlipuko wa hatari wa Ebola wa virusi aina ya Bundibugyo huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) unaendelea kuongezeka, huku juhudi za kuharakisha upimaji na kubaini matibabu yenye ufanisi zikiendelea, amesema Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) nchini humo, Dkt. Anne Ancia.

“Ukubwa halisi wa mlipuko huu bado haujafahamika kikamilifu, tungalipenda kusema kwamba hali inaanza kutulia, lakini kwa kweli, bado hatuwezi kusema hivyo,” amesema Dkt. Ancia, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, kwa njia ya video kutoka Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri ambalo ndio kitovu cha mlipuko huo.

Dkt. Ancia amesema kuanzia mwezi Mei mwaka huu mlipuko huo ulipotangazwa hadi tarehe 4 mwezi huu wa Julai:

  • Serikali imethibitisha wagonjwa 1,561 wenye Ebola
  • Kati yao 506 wamekufa na 254 wamepona.
  • Zaidi ya watu 10,000 waliokutana na wagonjwa wanaendelea kufuatiliwa.

Je WHO inafanya nini?

  • Linaimarisha uchunguzi wa historia ya kila mgonjwa ili “tuweze kuelewa kwa kina mlolongo wa maambukizi”
  • Kubaini wahusika
  • Kutenga watu wote waliokutana na wagonjwa.

Changamoto zilizopo

  • Vituo vya matibabu vimezidiwa uwezo
  • Hakuna magari ya kusafirisha wagonjwa

“Nilitembelea vituo vya matibabu ndani na karibu na mji wa Bunia, jimboni Ituri, na Beni, Butembo na Katwa jimboni Kivu Kaskazini, na nilijionea kujitolea kwa wafanyakazi ambao wanaendelea kuwahudumia wananchi wao licha ya changamoto kubwa,” amesisitiza.

Mlipuko wa sasa umeendelea katika maeneo yenye mapigano, watu waliokimbia makazi yao, na huduma za afya zilizoelemewa.

Kinachotia moyo

  • Upimaji umeongezeka kutoka vipimo 30 mjini Kinshasa hadi zaidi ya vipimo 2,000
  • Sababu ni maabara 10 zilizogawanywa katika majimbo yaliyoathirika na Ebola
  • Maabara ya hivi karibuni zaidi imefunguliwa Bunia.
  • Jaribio fanisi la kitabibu dhidi ya Ebola ya Bundibugyo limeanza Julai 2
  • Jaribio hilo litatathmini matibabu mawili yenye matumaini makubwa:
    • Kingamwili iitwayo MBP134
    • Dawa ya kuzuia virusi remdesivir

Dawa hizi zitatolewa zikiwa peke yake au kwa pamoja ili kutathmini uwezo wake wa kuongeza nafasi ya kuishi kwa wagonjwa wa Ebola ya aina ya Bundibugyo,” amesema.

  • Zaidi ya dozi 1,200 za matibabu zinapatikana kwa sasa
  • Matibabu mengine yanaweza kujumuishwa katika jaribio hilo kadiri ushahidi mpya wa kisayansi unavyojitokeza.

Madai ya M23 kuwa Ebola imetokomezwa kwenye maeneo inayodhibiti

Dkt. Ancia amethibitisha kuwa WHO imepokea taarifa zinazoonesha kwamba hakukuwa tena na wagonjwa wa ebola kwenye maeneo yanayodhibitiwa na M23 na kwamba “watu wote waliokuwa chini ya ufuatiliaji baada ya kukutana na wagonjwa walikuwa wameondolewa kwenye uangalizi huo.”

Maeneo hayo ni pamoja na Goma, jimboni Kivu Kaskazini, na Uvira, Bukavu na Sake jimboni Kivu Kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *