Programu hiyo imezinduliwa katika makao makuu ya FAO mjini Roma Italy , wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa ‘Kilimo Janja’ uliowakutanisha mawaziri, watunga sera, watafiti na wadau kutoka sekta binafsi kujadili namna teknolojia za kidijitali zinavyoweza kuboresha uzalishaji wa chakula duniani.

Udongo ndio msingi wa mavuno bora

FAO inasema taarifa sahihi kuhusu udongo zinaweza kuwa msingi wa kuongeza uzalishaji wa kilimo, kupunguza hatari ya mazao kushindwa na kusaidia wakulima kutumia rasilimali kwa ufanisi zaidi. Tathmini ya majaribio iliyofanyika katika Mkoa wa Kusini mwa Zambia ilionesha kuwa mashamba mawili yaliyopokea mvua sawa na kutumia mbinu zilezile za kilimo yanaweza kutoa matokeo tofauti kabisa kutokana na tofauti za aina ya udongo. Mahindi yalibainika kutofaa katika udongo wa aina ya udongo wa mawe au changarawe, lakini yalistawi vizuri katika udongo wa aina ya mfinyanzi  hali inayoonesha jinsi sifa za udongo zinavyoathiri mafanikio ya kilimo.

Akizungumzia umuhimu wa mfumo huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ardhi na Maji wa FAO, Lifeng Li, anasema teknolojia haiwezi kuchukua nafasi ya wakulima bali huwapa taarifa bora zinazowawezesha kufanya maamuzi sahihi kwa wakati na katika maeneo yanayofaa. Anaongeza kuwa changamoto kubwa sasa si kuthibitisha uwezo wa kilimo janja, bali kuhakikisha teknolojia hizo zinawafikia wakulima wanaozihitaji zaidi.

© FAO/Samuel Creppy Shule za vitendo za wakulima wa mashambani zinashughulikia masuala mengi kwa wakati mmoja: uhaba wa maji, afya ya udongo, utofauti wa mazao na utunzaji wa mifugo.

Jinsi CropSuit inavyofanya kazi

CropSuit huunganisha taarifa kuhusu udongo, hali ya hewa, topografia, matumizi ya ardhi na mahitaji ya mazao ili kutathmini mazao yanayoweza kustawi vizuri katika eneo husika kabla ya wakulima kuwekeza katika uzalishaji. FAO inasema takribani watu bilioni 1.7 duniani wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na uharibifu wa ardhi unaopunguza uzalishaji wa kilimo, hivyo matumizi ya taarifa sahihi yanaweza kusaidia wakulima kukabiliana na changamoto hizo na kuongeza usalama wa chakula.

Programu hiyo ni sehemu ya mradi wa Soil Mapping for Resilient Agrifood Systems (SoilFERyaani Ramani za Udongo kwa Mifumo Himilivu ya Chakula na Kilimo unaofadhiliwa na serikali za Japan na Marekani, na unajengwa juu ya mfumo wa Global Agro-Ecological Zoning (GAEZ) ulioanzishwa kwa ushirikiano kati ya FAO na Taasisi ya Kimataifa ya IIASA. Kwa sasa, miradi ya SoilFER inatekelezwa nchini Ghana, Guatemala, Honduras, Kenya na Zambia, ikilenga kuimarisha mifumo ya kitaifa ya taarifa za udongo, kuboresha huduma za ugani na kutoa mapendekezo ya kisayansi kuhusu mbolea, uchaguzi wa mazao na usimamizi wa ardhi.

Mafanikio nchini Zambia

Nchini Zambia, uchambuzi wa ramani za udongo na taarifa za mvua umeonesha kuwa ingawa mahindi yanafaa katika baadhi ya mashamba, maeneo jirani yanafaa zaidi kwa mazao kama muhogo, kunde na fonio jambo linalofungua fursa za kubadilisha mazao na kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Mratibu wa Kitaifa wa mradi wa SoilFER katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Zambia (ZARI), Rodgers Kabiti, amesema programu hiyo inawapatia wakulima, maafisa ugani, watafiti na wapangaji wa maendeleo taarifa zinazotegemea ushahidi wa kisayansi ili kuwasaidia kufanya maamuzi bora kuhusu uchaguzi wa mazao na usimamizi wa rutuba ya udongo.

Naye mtaalamu wa FAO wa Ukandaji wa Kilimo na Ikolojia, mmoja wa wabunifu wa CropSuit, Rutendo Mukaratirwa, amesema mfumo huo umeundwa kuunganisha taarifa za udongo, hali ya hewa, topografia na mahitaji ya mazao katika jukwaa moja linalorahisisha kutambua vikwazo vya uzalishaji na kupendekeza mazao yanayofaa kwa kila eneo, na kwamba unaweza kuboreshwa kadiri unavyoendelea kutumika.

FAO inasisitiza kuwa kabla ya wakulima kuamua aina ya mbolea, mbegu au mfumo wa umwagiliaji, swali la kwanza linapaswa kuwa iwapo zao walilochagua linaendana na aina ya udongo wa eneo husika  jibu ambalo linaweza kuamua mafanikio ya uzalishaji na mustakabali wa usalama wa chakula.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *