Dar es Salaam. Hali imeanza kuchangamka nje ya geti katika Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, wilayani Temeke huku idadi ya wananchi wanaofika kushiriki maonyesho hayo ikiendelea kuongezeka kadri muda unavyosonga.

Hali hiyo ni tofauti na ilivyokuwa mapema asubuhi, ambapo watembeleaji maonyesho hayo walikuwa wachache. Kwa sasa, misururu mirefu ya wananchi imeonekana wakisubiri kukaguliwa kabla ya kuruhusiwa kuingia ndani ya viwanja vya maonyesho hayo.

Hadi habari hii inaandikwa saa 6:31 mchana, leo  Julai 7, 2026, foleni za wananchi wanaotaka kuingia katika viwanja hivyo zimeendelea kuongezeka na kusogea hadi Barabara ya Kilwa pamoja na Kituo cha Mabasi ya Mwendokasi cha Sabasaba.

Hali ilivyo kiusalama

Magari ya Polisi yameonekana yakirandaranda katika mitaa mbalimbali inayozunguka viwanja hivyo, huku askari wakiendelea na doria za miguu katika maeneo tofauti kwa lengo la kuhakikisha usalama wa wafanyabiashara, washiriki na wananchi wanaotembelea maonyesho hayo unaendelea kuimarika.

Uimarishaji wa ulinzi na doria katika viwanja hivyo ulianza tangu mwishoni mwa wiki, ikiwa ni sehemu ya hatua zinazolenga kudumisha amani, utulivu na usalama wakati wote wa maonyesho hayo.

Ukitokea uhasibu Polisi pamoja na wanajeshi wamekita kambi wakiwa wamezunguka kwa muundo wa pembe tatu ukitokea Uwanja wa Taifa wamesimama upande wa kushoto, ukitokea Kigamboni wapo upande wa kulia lakini kama unaenda Sabasaba askari wengine wamekaa kulia.

Ukikaribia Viwanja hivyo ukitokea Uhasibu kuna gari ya washawasha na ikiwa unatokea upande wa kwa Azizi Ali kwenye makutano kuna askari wametanda kila kona.

Imeandikwa na Tuzo Mapunda

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *