Kwa Dkt. Caroline Asiimwe, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC) na mjumbe wa timu ya wataalamu ya UNESCO ya Kamusi ya Akili Mnemba ya Kiingereza–Kiswahili, nguvu kubwa ya Kiswahili ipo katika uwezo wake wa kuwaunganisha watu huku kikihifadhi utofauti.

“Kiswahili kimejengwa kwa namna ya kipekee kama alama ya umoja, amani na uelewano wa pamoja,” anasema. “Kwa sababu hakimilikiwi na kabila moja, kinaunda nafasi isiyo na upendeleo wa lugha ambapo tamaduni tofauti zinaweza kukutana bila ubabe wa lugha.”

UN News/Leah Mushi Dkt. Fillipo Lubua akieleza kuhusu suala la ChatGPT katika Kongamano la 8 la Kimataifa la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), huko jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania. (Maktaba)

Kiswahili kilichotokana na karne nyingi za mwingiliano katika pwani ya Afrika Mashariki, kimekuzwa kupitia biashara, mabadilishano ya kitamaduni na ushirikiano. Katika historia yake yote, kimekopa msamiati kutoka jamii mbalimbali huku kikihifadhi utambulisho wake wa Kiafrika, na hivyo kuwa mfano hai wa mazungumzo ya kitamaduni.

Leo, lugha hii ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiimarisha ushirikiano wa kikanda huku ikiunga mkono matumizi ya lugha nyingi. Tangu Novemba 2025, pia imekuwa lugha rasmi ya saba ya Mkutano Mkuu wa UNESCO, ikiungana na Kiarabu, Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kirusi na Kihispania. Badala ya kuchukua nafasi ya lugha za asili, Dkt. Asiimwe anaamini Kiswahili kinazisaidia kwa kuwezesha watu kutumia lugha zao za mama ndani ya jamii zao, Kiswahili kwa mawasiliano ya kikanda, na lugha za kimataifa kwa mawasiliano ya kimataifa.

Kuimarisha lugha nyingi kupitia ubunifu wa kidijitali

Wakati akili mnenba (AI) ikibadilisha jamii, UNESCO inafanya kazi kuhakikisha lugha za Afrika zinakuwa sehemu ya mustakabali wa kidijitali. Mwaka 2025, UNESCO ilizindua Kamusi ya Akili mnemba ya Kiingereza–Kiswahili, iliyotengenezwa kupitia mchakato wa ushirikiano uliowahusisha wanaisimu, wataalamu wa AI na wataalamu wa lugha. Rasilimali hii ya mtandaoni inayobadilika inaeleza na kutafsiri istilahi muhimu za akili mnemba hadi sasa ikiwa na istilahi 109 za msingi za AI kwa Kiingereza na Kiswahili, ikiwasaidia wanafunzi, walimu, watafiti, watunga sera na wavumbuzi kuelewa dhana za AI zinazobadilika kwa kasi kwa njia rahisi na inayofikika.

Akiwa mjumbe wa timu ya wataalamu ya UNESCO iliyochangia kamusi hiyo, Dkt. Asiimwe anasema mpango huo ni zaidi ya kamusi ya kawaida. “Kamusi za jadi zinanasa lugha iliyosimama, kamusi hii ya AI ni nyenzo hai inayobadilika,” anaeleza. Inavuka tafsiri ya moja kwa moja kwa kunasa muktadha, nahau na muktadha wa kitamaduni, ikisaidia kuhakikisha maana ya dhana haipotei.”

Kamusi hiyo pia inachangia juhudi pana za UNESCO za kupunguza vizuizi vya lugha katika ulimwengu wa kidijitali na kufanya teknolojia zinazoibuka ziwe rahisi kufikiwa na wazungumzaji wa lugha zisizo na rasilimali kubwa za kidijitali. Kwa kutoa istilahi sanifu za AI kwa Kiswahili, inaunga mkono elimu, utafiti, ubunifu na maendeleo ya AI yenye maadili katika eneo hili.

UNICEF Kenya Wasichana wa baraza la ushauri la vijana, Nairobi wakitazama app ya OKY.

Dkt. Asiimwe anasisitiza kuwa akili mnemba inaweza kuwa nyenzo yenye nguvu ya kuhifadhi na kukuza Kiswahili, iwapo itajengwa kwa kutumia data ya lugha ya ubora wa juu na inayohusiana na mazingira ya ndani.

Mifumo ya AI lazima ioneshe utajiri na mabadiliko ya Kiswahili,” anasema. “Hii inamaanisha kuendelea kujumuisha fasihi ya kisasa, vyombo vya habari, maoni ya jamii na misemo ya kikanda ili teknolojia iheshimu mazingira ya Kiafrika badala ya kutafsiri maneno tu.”

Lugha inayokua kimataifa

Utambuzi wa kimataifa wa Kiswahili unaakisi kuongezeka kwa ushawishi wake zaidi ya Afrika. Lugha hii inazidi kufundishwa katika vyuo vikuu duniani, na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kitaaluma, mabadilishano ya kitamaduni na ushirikiano wa kiuchumi.

Kwa wazungumzaji wengi, kuongezeka kwa umaarufu huu pia kunawakilisha kutambuliwa kwa thamani ya kiakili na kitamaduni ya lugha za Afrika.

Uteuzi wa Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili umehamasisha mashirika ya kimataifa, taasisi za elimu, wachapishaji na wavumbuzi wa kidijitali kuwekeza katika lugha hiyo.

Kulingana na Dkt. Asiimwe, UNESCO imekuwa na mchango mkubwa katika mabadiliko haya kwa kukuza Kiswahili kama lugha ya ujumuishi na mazungumzo. “Kimekipandisha Kiswahili kutoka kuwa lugha ya kikanda ya mawasiliano hadi kuwa chombo muhimu cha amani, maendeleo endelevu na urithi wa pamoja wa kitamaduni,” anasema.

Wakati UNESCO ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili, Shirika hilo linathibitisha tena kujitolea kwake kwa lugha nyingi na utofauti wa lugha kama msingi muhimu wa jamii jumuishi za maarifa. Katika zama za kidijitali, mipango kama Kamusi ya Akili mnemba ya Kiingereza–Kiswahili inaonesha jinsi teknolojia inavyoweza kulinda lugha huku ikipanua upatikanaji wa elimu, ubunifu na mazungumzo ya kitamaduni.

John Kibego Dkt. Caroline Asiimwe, mmoja wa watafiti wa matumizi ya lugha ya Kiswahili duniani wakati alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Makerere.

Kwa Dkt. Asiimwe, dira iko wazi: “Kiswahili kinapaswa kuwa mstari wa mbele katika mabadiliko ya kidijitali ya kimataifa. Kinapopanuka katika majukwaa ya kimataifa, kinaweza kukuza uelewano wa kina kati ya tamaduni, kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuhakikisha sauti za Afrika zinakuwa washirika sawa katika kuunda mustakabali wetu wa kidijitali wa pamoja.”   

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *