
Shirikisho la Soka Uholanzi (KNVB) limeanza mazungumzo na Meneja wa zamani wa Liverpool, Arne Slot ili awe Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya nchi hiyo.
KNVB inamuona Slot kama mtu sahihi wa kurithi mikoba ya Ronald Koeman ambaye alibwaga manyanga muda mfupi baada ya Uholanzi kutolewa na Morocco katika Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Kwa sasa Slot hana timu anayoifundisha tangu alipotupiwa virago na Liverpool baada ya msimu wa 2025/2026 kumalizika.
Kocha huyo alitimuliwa msimu mmoja tu baada ya kuiongoza Liverpool kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL).
Slot mwenye umri wa miaka 47, amewahi pia kuzinoa Cambuur, AZ Alkmaar na Feyenoord kabla ya kujiunga na Liverpool.
Inaripotiwa pia Kocha mwingine anayepigiwa chapuo kumrithi Koeman ni Meneja wa zamani wa Manchester United, Eric Ten Hag.
Koeman alijiuzulu kuinoa Uholanzi, Julai Mosi, saa chache baada ya timu yake kuchapwa na Morocco kwa mikwaju ya penalti 3-2 katika mechi ya hatua ya 32 Bora.