
Kikao hicho kimefanyika chini ya ajenda ya “Vitisho kwa Amani na Usalama wa Kimataifa.” Waliozungumza ni pamoja na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani, Rosemary DiCarlo, na Msaidizi wa Katibu Mkuu upande wa Masuala ya Kibinadamu, Indrika Ratwatte. Wawakilishi wa Ukraine, nchi kadhaa za eneo hilo na Umoja wa Ulaya pia wamehudhuria.
Mawimbi matatu ya mashambulizi makubwa
“Katika wiki moja pekee iliyopita, mawimbi matatu makubwa ya mashambulizi ya anga ya Urusi yameikumba Kyiv na miji mingine ya Ukraine, na kusababisha ongezeko la kutisha la vifo vya raia pamoja na uharibifu mkubwa,” amesema DiCarlo.
Ameeleza kuwa usiku wa Julai 8, Kyiv, Kharkiv na Odesa zilishambuliwa. Siku chache kabla ya hapo, usiku wa Julai 6, Kyiv na eneo la Kyiv zililengwa na makombora kadhaa, yakiwemo ya balistiki, cruise na hypersonic, pamoja na mamia ya droni. Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa, watu wasiopungua 28 waliuawa, akiwemo mvulana mwenye umri wa miaka 12, huku zaidi ya 90 wakijeruhiwa, wakiwemo watoto saba.
DiCarlo pia amekumbusha kuwa usiku wa Julai 2, vikosi vya Urusi vilirusha zaidi ya makombora 70 na karibu droni 500 kuelekea Kyiv. Takribani watu 31 waliuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa. Zaidi ya wakazi 50,000, wakiwemo maelfu ya watoto, walijificha katika vituo vya metro (tren iza chini ya ardhi). Uharibifu uliripotiwa katika wilaya zote za mji mkuu pamoja na maeneo ya Mykolaiv, Zaporizhia, Chernihiv na Dnipropetrovsk. Aidha, shambulizi dhidi ya kituo cha afya mjini Kherson lilimuua daktari mmoja na kumjeruhi muuguzi.
“Mwelekeo unaoendelea”
DiCarlo amesema mashambulizi hayo yanaonesha mwenendo unaojirudia.
“Mashambulizi haya yanaonesha mtindo ulio wazi. Yamelenga miji mikubwa yenye idadi kubwa ya raia. Majengo ya makazi yameharibiwa au kuathiriwa vibaya, jambo lililosababisha madhara makubwa kwa wakazi wake. Tunayalaani mashambulizi haya kwa nguvu zote,” amesema.
Hali katika maeneo yanayokaliwa na Urusi
DiCarlo amesema kuongezeka kwa mapigano kunaendelea kuwaathiri raia katika maeneo ya Ukraine yanayokaliwa kwa muda na Shirikisho la Urusi pamoja na maeneo mengine yaliyo karibu na mstari wa mbele.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa, shambulizi la droni katika soko kuu la Tokmak, mkoani Zaporizhzhia unaokaliwa na Urusi, tarehe 3 Julai liliua angalau raia watano na kuwajeruhi wengine 21. Aidha, Julai 6, shambulizi linalodhaniwa kufanywa na Ukraine katika eneo la Crimea linalokaliwa na Urusi lilisababisha kifo cha mtu mmoja na kukatika kwa umeme kwa kiwango kikubwa. Mamlaka za Urusi katika Crimea na Sevastopol zilitangaza hali ya dharura kutokana na upungufu wa mafuta na maji.
DiCarlo pia amesema Ukraine imeendelea kufanya mashambulizi ya droni dhidi ya miundombinu ya mafuta, viwanda na malengo ya kijeshi ndani ya Urusi, huku baadhi ya mashambulizi hayo yakiripotiwa kusababisha vifo vya raia na uharibifu wa mali za kiraia.
Kwa mujibu wa mamlaka za Urusi, shambulizi la droni linalodhaniwa kufanywa na Ukraine katika eneo la Belgorod tarehe 2 Julai lilimuua mtu mmoja na kusababisha kukatika kwa huduma za maji na umeme. Siku hiyo hiyo, mamlaka za Bryansk ziliripoti kifo kingine kutokana na shambulizi linalodhaniwa kufanywa na Ukraine.
Mei 2026 mwezi wenye vifo vingi zaidi vya raia
DiCarlo amesema kwa mujibu wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu (OHCHR), mwezi Mei ulikuwa mwezi ulioshuhudia vifo vingi zaidi vya raia nchini Ukraine tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi mwaka 2022. Takwimu za awali za Juni zinaonesha hali imekuwa mbaya zaidi, zikiwa na angalau watu 265 waliouawa na 1,816 kujeruhiwa.
Tangu Februari 2022, Umoja wa Mataifa umethibitisha vifo vya angalau raia 16,402, wakiwemo watoto 802, huku zaidi ya watu 48,000 wakijeruhiwa. Umoja wa Mataifa unasema idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi.
Wito wa kusitishwa kwa mapigano
Akihitimisha hotuba yake, DiCarlo amesisitiza umuhimu wa suluhisho la kidiplomasia.
“Usitishaji wa mapigano wa haraka, kamili na usio na masharti haupaswi kucheleweshwa tena. Unapaswa kuwa hatua kuelekea amani ya haki, ya kudumu na ya kina kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa,” amesema.
Mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka
Kwa upande wake, Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Masuala ya Kibinadamu, Indrika Ratwatte, amesema mamia ya raia wameuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyotokea wiki iliyopita.
“Mbali na miji mikubwa, watu wanaoishi karibu na maeneo ya mapigano wanaendelea kuishi katika tishio la kila siku, hali kadhalika raia walioko katika maeneo yanayokaliwa na Shirikisho la Urusi,” amesema Ratwatte akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu, Tom Fletcher.
Pia ameonesha wasiwasi kuhusu taarifa za vifo vya raia na uharibifu wa miundombinu ndani ya Urusi.
Kazi ya mashirika ya misaada yazidi kuwa hatarini
Ratwatte amesema mashirika ya misaada yanakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kuwafikia wanaohitaji msaada. Katika baadhi ya maeneo ya Donetsk, upatikanaji wa misaada unazuiwa mara kwa mara, jambo linalochelewesha uokoaji wa raia na usambazaji wa misaada muhimu.
Ameongeza kuwa mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada yanaongezeka. Wiki iliyopita, droni ilishambulia msafara wa misaada katika eneo la Dnipropetrovsk, ikiwa ni tukio la tatu la aina hiyo ndani ya miezi miwili. Shambulizi jingine liliharibu ghala la Shirika la Msalaba Mwekundu la Ukraine.
“Kwa ujumla, idadi ya mashambulizi yaliyosababisha majeraha kwa wahudumu wa misaada na uharibifu wa mali zao imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita,” amesema.
Ratwatte amekumbusha kuwa sheria za kimataifa zinazitaka pande zote katika mzozo kuwalinda raia, wahudumu wa misaada na miundombinu ya kiraia, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia waathirika bila vikwazo.
“Bila kujali kasi ya juhudi za kisiasa, raia hawawezi kusubiri. Mahitaji yao ni ya dharura na yanaongezeka. Wanahitaji ulinzi na msaada sasa. Ninawasihi wajumbe wa Baraza hili kutumia ushawishi wao kutafuta njia zote zinazowezekana za kuzuia mateso zaidi kwa raia,” amesema Ratwatte.