Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imefanikiwa kufanya kwa mara ya kwanza upasuaji wa moyo kwa njia ya matundu kwa watoto watatu kutoka Burundi, hatua inayotajwa kuimarisha uwezo wa Tanzania katika kutoa huduma za kibingwa na kukuza utalii wa matibabu barani Afrika.

Upasuaji huo umefanywa kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ukiwa sehemu ya juhudi za kujenga uwezo wa ndani wa kutoa huduma za matibabu ya moyo na kupanua huduma kwa wagonjwa kutoka nje ya nchi.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo leo Alhamisi, Julai 9, 2026 hospitalini hapo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abeli Makubi amesema hatua hiyo inaendana na ajenda ya Serikali ya kuendeleza utalii wa matibabu kwa kuvutia wagonjwa kutoka nchi jirani na mataifa mengine kupata huduma za kibingwa nchini, badala ya kusafiri nje ya Afrika.

Tumekamilisha upasuaji wa moyo kwa watoto watatu kutoka Burundi. Hii inaonyesha jinsi tunavyoweza kutumia utaalamu tulionao kuwahudumia Watanzania na wakati huohuo kupanua nafasi ya nchi yetu katika kutoa huduma kwa wagonjwa kutoka nje ya Tanzania,” amesema Profesa Makubi.

Picha ya wadau wa mazingira kwenye uzinduzi wa mpango wa usimamizi wa mazingira kwenye sekta ya kilimo (ASEAP II) Jijini Dodoma leo Julai 9, 2026

Amesema upasuaji huo umehusisha kuziba matundu ya moyo kwa watoto watatu, huku watoto wengine waliopimwa wakipatiwa matibabu mbadala baada ya kubainika kuwa hali zao hazikukidhi vigezo vya kitaalamu vya kufanyiwa upasuaji huo, kutokana na ukubwa wa athari za ugonjwa.

Profesa Makubi amesema awali huduma hiyo ilikuwa ikitolewa kwa watu wazima pekee, lakini kutokana na kuimarika kwa uwezo wa hospitali, sasa imeanza kutolewa pia kwa watoto.

“Kwa sasa hospitali yetu inatoa huduma za magonjwa ya moyo kwa viwango vya kitaifa na kimataifa, ikiwamo uwekaji wa vifaa vya kusaidia mapigo ya moyo kwa wagonjwa wenye mapigo hafifu na upasuaji wa kuziba matundu ya moyo kwa watu wazima. Sasa tumepanua huduma hiyo kwa watoto,” amesema.

Ameongeza kuwa, kuimarika kwa huduma hizo kumechangia kupunguza idadi ya Watanzania wanaolazimika kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu ya moyo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Tiba Utalii Tanzania, Dk Asha Mahita amezitaka taasisi za afya nchini kuendelea kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ili kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na sekta ya utalii wa matibabu.

Amesema ushirikiano huo pia utawasaidia Watanzania kupata huduma hizo ndani ya nchi kwa gharama nafuu kuliko ilivyokuwa wanapolazimika kwenda kutibiwa nje ya Tanzania.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka JKCI, Godwin Sharao amesema kuhudumia wagonjwa kutoka mataifa mengine kutasaidia kuendelea kuboresha ubora wa huduma za matibabu nchini.

Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao kutoka wizara ya kilimo Dk Yasinta Msogela akizungumza kwenye uzinduzi wa mpango wa usimamizi wa mazingira wa sekta ya kilimo wa miaka mitano (ASEAP II)  Jijini Dodoma leo Julai 9, 2026

Amesema huduma kwa wagonjwa wa kimataifa huwapa wataalamu fursa ya kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuongeza ushindani wa kitaaluma.

Tukiweza kuwahudumia wagonjwa wetu hapa nchini, tutaokoa fedha na muda ambao ungepotea kwa kufuata matibabu nje ya nchi. Wakati huohuo tutajenga wataalamu wenye ushindani mkubwa na kuongeza uwezo wa Tanzania kuvutia wagonjwa kutoka mataifa mengine,”amesema Dk Sharao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *