Dar es Salaam. Wanawake 18 vijana wanaofanya kazi katika sekta ya nishati ya nyuklia na teknolojia za hali ya juu kutoka nchi 11, Tanzania ikiwemo, wamehitimu mafunzo ya kimataifa ya uongozi yaliyofanyika nchini Russia chini ya mpango wa inVisible Power Leadership Camp.
Mafunzo hayo ya wiki moja yaliandaliwa na Rosatom Corporate Academy kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).
Hii ni mara ya kwanza kwa taasisi hizo kushirikiana kuendesha programu hiyo tangu ilipoanzishwa miaka mitatu iliyopita.
Akizungumza katika hafla ya kuwatunuku vyeti washiriki iliyofanyika Julai 2, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Rosatom Corporate Academy, Yulia Uzhakina amesema programu hiyo imewapa fursa wahitimu hao ya kuongeza maarifa, kupanua mitandao ya kitaaluma na kujiandaa kwa hatua zinazofuata katika taaluma zao.
“Ninafurahi kuwapongeza kwa kukamilisha mafunzo na kupokea vyeti vyenu. Nina imani kuwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita mmepata maarifa muhimu, mmejenga mitandao ya kitaaluma na mmechukua hatua muhimu katika kujenga mwelekeo wa taaluma zenu. Inatia moyo kuona wanawake wenye vipaji na dhamira wakichangia mustakabali wa sekta ya kisasa ya nishati ya nyuklia,” amesema Uzhakina.
Amesema washiriki wa mwaka huu wametoka Bangladesh, China, Colombia, Misri, India, Indonesia, Kyrgyzstan, Afrika Kusini, Tanzania, Uturuki na Uzbekistan.
Amesema mafunzo hayo yalianza rasmi Juni 25 na kuhitimishwa Julai 2, 2026 katika miji ya Obninsk na Moscow nchini Russia.
Akizungumzia mafunzo hayo, mshiriki kutoka mamlaka ya mitambo ya kuzalisha umeme kwa nyuklia kutoka Misri, Nada Adel Salah Attia amesema programu hiyo imempa nafasi ya kujifunza na kujenga uhusiano wa kitaaluma na washiriki kutoka mataifa mbalimbali.
“Haikuwa tu kuhusu kupata maarifa, bali pia kukua kupitia watu, mazungumzo na uzoefu tuliokuwa tukishirikiana,” amesema.
Mbali ya kujifunza darasani, washiriki walipata wasaa wa kushiriki mihadhara ya kitaalamu, warsha za vitendo pamoja na majadiliano ya kubadilishana uzoefu na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zinazoongoza katika sekta hiyo.
Miongoni mwa wakufunzi na washauri waliotoa mihadhara na mafunzo ni pamoja na Pedro Dieguez Porras na Lisa Lande kutoka IAEA, Polina Lion kutoka Rosatom State Corporation, Elsie Pule kutoka BRICS Nuclear Energy Platform, Sithembile Mbuyisa kutoka Shirika la Nishati ya Nyuklia la Afrika Kusini (NECSA) na Galina Bogdanova kutoka Rosatom Corporate Academy.
Wengine ni Alexandra Yustus, Ilya Platonov na Elizaveta Zatsepa kutoka Rosatom International Network pamoja na Alexandra Ryabykh kutoka Women in Nuclear Russia.
Attia anasema mwishoni mwa mafunzo, kila mshiriki alipatiwa nafasi ya kuandaa mkakati binafsi wa maendeleo ya taaluma yake.
Mpango wa inVisible Power Leadership Camp ni programu ya kimataifa inayofanyika kila mwaka ikilenga kuwaendeleza wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya nishati ya nyuklia kwa kuwajengea uwezo wa uongozi, kuwawezesha kupanga mikakati ya maendeleo ya taaluma zao na kupanua mitandao ya kitaaluma.