Taarifa iliyotolewa na ofisi yake jijini Geneva, Uswisi imeeleza kwamba katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, mapigano yameongezeka kati ya jeshi la DRC (FARDC) na kundi la waasi la M23 katika maeneo ya Fizi na Mwenga, jimbo la Kivu Kusini. Pande zote mbili zimetumia ndege zisizo na rubani (droni) zenye silaha, mizinga mizito na silaha nyingine za milipuko katika maeneo yenye raia wengi. Raia wengi wameuawa, wengine kujeruhiwa, huku mifugo na makazi yakiharibiwa.

“Inasikitisha sana kwamba licha ya makubaliano yaliyofikiwa kupitia michakato inayoendelea ya amani, mapigano yanaendelea bila kupungua mashariki mwa DRC, yakisababisha vifo, majeraha na watu kuhama makazi yao, pamoja na kuharibu maisha na vyanzo vyao vya kujikimu,” amesema Türk kufuatia mapigano makali yaliyotokea karibu na kijiji cha Mulima, Fizi, tarehe 4 na 5 Julai.

Ameongeza akisema, “ninayasihi majeshi ya DRC na M23 kuchukua hatua mara moja kusitisha ghasia zaidi na kupunguza mvutano haraka. Pia nazipa wito pande zote mbili kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda raia wa Mulima na eneo lote la nyanda za juu na za kati za Fizi na Mwenga. Matumizi ya silaha za milipuko zenye athari kubwa katika maeneo yenye watu wengi yana madhara makubwa na lazima yakome.”

Hofu inaongezeka

Mapigano yanayoendelea yanaweza kusababisha watu wengi zaidi kuhama makazi yao, wakiwemo wanaoweza kukimbilia nchi jirani, pamoja na kuongeza ukiukaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwemo mauaji yasiyo halali na ukatili wa kingono unaohusiana na mizozo.

“Pande zote katika mzozo huu pamoja na washirika wao zina wajibu wa wazi chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia kwa usalama, haraka na bila vikwazo wote wanaohitaji,” amesema Mkuu huyo wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa.

FDLR warudi kwao Rwanda

Aidha Bwana Türk ameisihi Rwanda kusitisha uungaji mkono wake kwa M23 na kuondoa wanajeshi wake kutoka DRC. Pia, amezitaka mamlaka za DRC kuongeza juhudi zao za kuwaondoa vitani, kuwanyang’anya silaha na kuwarejesha nchini mwao wanachama wa kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).

Türk amewataka pia wadau wa kikanda na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kuzuia kuongezeka kwa ghasia katika maeneo ya nyanda za juu na za kati ya Kivu Kusini, wakijenga juu ya juhudi za kisiasa na kidiplomasia zinazoendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *