Rais Masoud Pezeshkian amesema mahudhurio makubwa ya watu kutoka matabaka yote ya jamii katika mazishi makubwa yaliyofanyika kwa ajili ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ni kielelezo cha umoja wa kitaifa nchini Iran.

Akizungumza katika kikao cha baraza la mawaziri jana Jumatano, Pezeshkian alisema Wairani “waliunda tukio kubwa” kwa kujitokeza kwa mamilioni kwa ajili ya mazishi yaliyofanyika kutoa heshima na kumuenzi Ayatullah Khamenei katika mji mkuu Tehran na mji wa Qum mapema wiki hii.

“Ushiriki mkubwa na wa ajabu wa makundi yote ya watu ni onyesho la umoja, mshikamano, uratibu, mwingiliano, ushirikiano na usimamizi mzuri,” amesema Rais Pezeshkian na kuongeza kwamba mkusanyiko usio na kifani wa watu kwa ajili ya mazishi ya Ayatullah Ali Khamenei umekuwa kama “ngao dhidi ya vitisho vya Marekani na maadui wengine.”

“Kwa mbinu hii ya usimamizi na uongozi, tutasonga mbele na tutavuruga ndoto za maadui kupitia umoja wa kitaifa na mshikamano uliopo ndani ya jamii,” amesisitiza Daktari Pezeshkian.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliuawa shahidi katika shambulio la anga akiwa ofisini kwake mjini Tehran mnamo Februari 28, siku ya kwanza ya mashambulizi ya kushtukiza ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambayo yalisimamishwa kwa kusitisha mapigano mapema mwezi Aprili.

Baada ya shughuli kubwa ya mazishi iliyofanyika jana katika miji mitakatifu ya nchi jirani ya Iraq, mwili wa hayati Imam Khamenei leo utakuwa katika mji wa kaskazini mwa Iran wa Mash’had, na baada ya kuagwa na mamilioni ya wakazi wa mji huo na mikoa ya kandokando hatimaye kiongozi huyo atazikwa katika Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Ali bin Musa Ridha (AS).  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *