
Bi. Rossbach amesema dunia imepiga hatua katika maeneo kama usafiri wa umma, upangaji wa miji na ukusanyaji wa taka, lakini akaonya kuwa sakata la makazi linaloikabili dunia linadhoofisha juhudi za kujenga miji jumuishi na yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Mambo muhimu yaliyoainishwa kwenye ripoti
- Zaidi ya watu bilioni 1 wanaishi katika makazi duni na yasiyo rasmi, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya watu milioni 130 tangu mwaka 2015.
- Takribani watu bilioni 3 duniani hawana makazi bora.
- Karibu nusu ya kaya zote duniani hutumia zaidi ya asilimia 30 ya mapato yao kulipa kodi ya nyumba, huku bei za nyumba zikiendelea kupanda kwa kasi kuliko ongezeko la kipato.
- Ripoti inaeleza kuwa makazi si mahali pa kuishi pekee, bali pia huamua upatikanaji wa usafiri, ajira, elimu, huduma za afya na huduma nyingine muhimu.
Bi. Rossbach amesema katika hali hii wanaodhurika zaidi ni wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu, wahamiaji, na watu waliolazimika kuhama makazi yao na wakazi wa makazi duni.
Kenya na inachofanya kusongesha SDG11 hasa kwenye makazi
Katika mkutano huo, Kenya ambayo ni mwenyeji wa UN_HABITAT imeelezea jinsi inavyokabiliana na changamoto ya makazi.
Mwakilishi wake wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Erastus Ekitela Lokaale amesema Kenya inaamini kuwa makazi ya gharama nafuu ni msingi muhimu wa kufanikisha miji endelevu.
- Zaidi ya nyumba 270,000 zimekamilika au ziko katika hatua za mwisho za ujenzi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
- Kupitia Mpango wa Makazi ya Gharama Nafuu, Kenya inalenga kupunguza upungufu wa takriban nyumba 250,000 unaojitokeza kila mwaka, huku ujenzi wa sasa ukiwa karibu nyumba 50,000 kwa mwaka.
Balozi Lokaale amebainisha kuwa Jukwaa la Miji la Afrika, lililofanyika Nairobi mwezi Aprili 2026, lilisisitiza umuhimu wa kuimarisha mamlaka za serikali za mitaa, kuongeza ufadhili endelevu, kukuza ubunifu, kuboresha matumizi ya takwimu na kuimarisha ushirikiano.
Hivyo amesema “nchi zibadili ahadi kuwa vitendo kwa kuimarisha uwezo wa serikali za mitaa, kuboresha mifumo ya takwimu za mijini, kuwekeza katika makazi ya gharama nafuu na kujenga miji inayoweza kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga mengine ya siku zijazo.”
Ametamatisha akisema kuwa, “Kama mwenyeji wa UN-Habitat, Kenya iko tayari kuendelea kushirikiana na nchi wanachama pamoja na wadau mbalimbali ili kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo na kuyageuza kuwa hatua halisi zinazoboresha maisha ya watu na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.