
Video iliyorekodiwa kutoka juu kwa teknolojia ya camera ya droni mjini Bunia jimboni Ituri, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC inaonesha Kituo cha Tiba dhidi ya Ebola katika Kituo cha Afya cha Evangelical, CME.
Sehemu ya iliyokuwa wodi ya watoto imegeuzwa kuwa kituo cha Ebola. Wahudumu wa afya wanaonekana wamevaa mavazi ya kujikinga na mavazi mengine ya namna hiyo yameanikwa nje yakaukwe kwa jua.
Dkt. Patrice Kabongo, Mratibu wa usimamizi wa wagonjwa, Ofisi ya Shirika WHO nchini DRC anafafanua zaidi walichokifanya hapa ili kuimarisha mapambano dhidi ya Ebola.
“Kuhusu kituo hiki, ni vyema kufahamu kwamba tulianza katika jengo moja; kulikuwa na wodi ya watoto iliyokuwa imejengwa tayari na Hospitali ya CME; jengo hilo la watoto halikuwa likitumika bado kwa sababu halikuwa limekabidhiwa rasmi kwa ajili ya matumizi. Hivyo, mlipuko ulipotokea, tuliona kuwa kulikuwa na fursa nzuri ya kuanzia hapo. Tulijaribu kurekebisha mpangilio na kufanya marekebisho kadhaa kulingana na hali ya majengo hayo ili tuweze kuanza kuwapokea wagonjwa haraka. Lakini ni lazima niseme kwamba ilikuwa changamoto kidogo kwa sababu, kwa vile majengo hayo hayakusanifiwa kwa ajili ya kutibu wagonjwa wa Ebola, hakukuwa na utaratibu wa kuruhusu familia kuingia na kuwatembelea wapendwa wao. Tulijenga haraka sehemu ya ziada. Hii ndiyo unayoiona hapa.”
Kupitia kidirisha cha karatasi ya plastiki kilichowekwa katika mlango uliotengenezwa kwa turubai, wagonjwa wa Ebola wanaonekana wakiwa kwenye vitanda wodini.
Dkt. Patrice Kabongo anaeleza zaidi akisema, “na kwa upanuzi huu, familia zinaweza kuja kuwatembelea wapendwa wao wagonjwa bila matatizo yoyote. Na sisi, kama wahudumu wa afya, tunaweza pia kuwatembelea na kuwafuatilia wagonjwa.” Dkt. Kabogo anasema hatua hiyo ya kuruhusu watu kuwaona japo kwa mbali jamaa zao imesaidia sana kuwapa watu imani na hata imeongeza utayari wa wagonjwa kuja wenyewe hospitali.
“Kwasababu hapo awali, hawakuelewa kinachoendelea ndani kwa kuwa hawakuruhusiwa kuingia. Na ilipotokea kifo au mgonjwa hali yake ilipokuwa mbaya, walikuja na nadharia za kila aina. Lakini sasa, wanaweza kujionea wenyewe jinsi ugonjwa unavyoendelea na hali ya wagonjwa; wanaingia ndani na hata pale kifo kinapotokea, kwa masikitiko, familia hutoa shukrani. Wanasema, ‘Tumeona kila kitu mlichofanya; tunaona jinsi mlivyomunganisha na mashine na vifaa vingine. Tunakushukuruni, na tutajitahidi kutoa elimu kwa wengine ili nao waweze kuja mapema zaidi.’”