Washindi wa Tuzo ya 41 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, (UNFPA) kwa mwaka 2026 ni Profesa Serigne Magueye Gueye, daktari bingwa wa upasuaji kutoka Senegal anayerejesha matumaini kwa manusura wa fistula ya uzazi, ilhali shirika la  Fondation Bonne Action Umugiraneza la Burundi limeibuka kidedea katika ngazi ya taasisi.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya UNFPA iliyotolewa Jumatano jijini New York, Marekani.

Profesa Serigne Gueye akizungumza jukwaani wakati wa sherehe ya tuzo UNFPA .

Umoja wa Mataifa Profesa Serigne Gueye, Mkuu wa Idara ya tiba ya magonjwa yahusianayo na njia ya haja ndogo katika Hospitali Kuu ya Grand Yoff nchini Senega, akizungumza baada ya kushinda Tuzo ya UNFPA ya 2026.

Profesa Serigne Magueye Gueye amefanya nini hadi kutunukiwa?

  • Amejitolea kuwasaidia wanawake kupona fistula ya uzazi, jeraha kubwa linalotokana na uzazi katika njia ya mkoojo, ambalo linaweza kuwaacha wanawake wakivuja mkojo au kinyesi bila kujizuia, kutengwa na jamii na kunyanyapaliwa.
  • Mbali na kuwahudumia wagonjwa mwenyewe, amewafundisha madaktari bingwa wa upasuaji kutoka zaidi ya nchi 45 za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara
  • Hatua hii imepanua upatikanaji wa huduma za matibabu zinazobadilisha maisha ya wanawake katika ukanda huo.
  • Dhamira yake haikuishia ndani ya chumba cha upasuaji pekee. Ili kuwafikia watu ambao wasingeweza kupata huduma za afya, Profesa Gueye aligeuza nyumba yake kuwa kituo cha afya kwa kuanzisha Kituo cha Afya cha Aristide Mensah huko Yeumbeul, kitongoji cha Dakar, mji mkuu wa Senegal.

Pia alikuwa miongoni mwa madaktari wa kwanza kuhimiza matibabu ya fistula katika Afrika Magharibi, akichangia kuongeza uelewa kuhusu tatizo hili ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuzuilika na kutibika iwapo wanawake watapata huduma bora za afya ya uzazi kwa wakati. Kupitia kazi yake kama daktari wa upasuaji, mwalimu na mtetezi wa afya, amesaidia kurejesha afya na heshima ya wanawake wengi.

Angeline Ndayishimiye akizungumza jukwaani wakati wa hafla ya UNFPA nchini Burundi.

Umoja wa Mataifa Angeline Ndayishimiye, ambaye ni Mke wa Rais wa Burundi na pia Mwanzilishi wa Fondation Bonne Action Umugiraneza, akizungumza baada ya kupokea Tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Afya ya Uzazi na Idadi ya watu ya mwaka 2026 jijini New York, Marekani.

Na vipi kuhusu Fondation Bonne Action Umugiraneza ya Burundi?

  • Hii inafanya kazi ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na msaada wa kijamii kwa wanawake, watoto na familia zilizo katika mazingira magumu zaidi nchini humo.
  • Programu zake zinalenga kupanua upatikanaji wa huduma muhimu na kushughulikia vikwazo vinavyochangia afya duni, ukosefu wa usawa na ukatili wa kijinsia.
  • Mwaka 2022, taasisi hiyo ilifungua Polyclinique Umugiraneza katika jimbo la Gitega, na hivyo kusogeza karibu na jamii za vijijini huduma za kibingwa za kitabibu, zikiwemo huduma za watoto, matibabu ya dharura na huduma za uzazi.
  • Imesaidia watoto waliozaliwa na matatizo makubwa kupata upasuaji unaookoa maisha.
  • Imetoa huduma kwa wanawake wanaoishi na fistula ya uzazi
  • Imeanzisha shule ya Socle du Savoir, inayochanganya elimu, lishe na uhamasishaji kuhusu hatari za ujauzito wa utotoni.
  • Hutoa hifadhi na huduma za msaada kwa manusura wa ukatili wa kijinsia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *