Mbeya. Pamoja na migahawa kuwainua wengi kiuchumi na kusaidia kundi kubwa kwenye jamii, wakiwemo wageni na wenyeji, ndani yake kuna mwiba mkali kutokana na baadhi kutozingatia sheria na taratibu za uendeshaji na hivyo kutishia afya kwa wananchi.

Ni wazi kuwa migahawa imekuwa msaada mkubwa kwa wajasiriamali ambao mbali na kujipatia kipato, wamekuwa wakiichangia Taifa kuinua maendeleo.

Kutokana na mafanikio yanayopatikana kupitia shughuli hiyo kwa sasa idadi yake inazidi kuongezeka kila siku, ambapo wengine wamekuwa wakitumia njia zisizo rasmi kufanya kazi hiyo ilhali kujiapatia kipato.

Sheria inaelekeza kabla ya mtu yeyote kuanza biashara ya mghahawa, lazima afanye vipimo vya afya katika vituo vya afya vilivyoainishwa na Serikali na kupewa cheti maalumu cha kumruhusu kufanya kazi hiyo.

Picha  zikionesha mama kishe wakiendelea na shughuli zao za migahawa katika maeneo tofauti ya Sokoine jijini Mbeya

Mbali na mmiliki wa mgahawa, pia wahudumu wake wanapaswa kupima afya zao ili kufanya huduma inayotolewa kwa walaji, iwe imethibitishwa kitaalamu kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza kiafya.

Wataalamu wanafafanua kuwa kufanya biashara hiyo bila kukidhi vigezo kiafya, kunaweza kuleta athari kwa walaji kutokana na maandalizi ya chakula, kuanzia mazingira hadi kumfikia mlaji.

Pia, wananchi wametahadharisha baadhi ya migahawa haiko salama kutokana na mazingira na huduma inayotolewa kuhatarisha afya zao, wakiomba mamlaka kufanya uchunguzi na kuwabaini.

Katika uchunguzi wa Mwananchi ilioufanya katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mbeya, imebaini idadi kubwa ya mama na baba lishe kuongezeka, huku wakiwa hawana uelewa juu ya sheria za kazi hiyo.

Mbali na migahawa, kumekuwapo na wimbi la vijiwe vya nyama choma, chipsi katika maeneo ya stendi, ambavyo kwa ujumla havikidhi ubora wa afya.

Wakizungumza na gazeti kwa nyakati tofauti baadhi ya wauzaji chakula wamekiri kupima afya zao na kuruhusiwa kufanya shughuli hizo, huku wengine wakikiri kutojua iwapo kuna utaratibu unapaswa kufanyika.

Picha zikionesha mama lishe wakiendelea na shughuli zao za migahawa katika maeneo tofauti ya Sokoine jijini Mbeya

Victoria Michael ambaye ni mama lishe wa Uyole amesema tangu aanze shughuli za kuuza chakula miaka sita sasa, hajui kama kuna utaratibu wowote wa kufanya ili kuendesha biashara hiyo.

“Binafsi we ndio unaniambia kuhusu kupima, kwa hiyo tunapima wapi? Nani anatuthibitisha kwamba afya zetu ni nzuri au wanapima ugonjwa gani ili mtu ajue afanye biashara hii au asifenye.

“Yaani hata sikuelewi naona kama unanipa hofu tu ila kwa ujumla nijuavyo ni kulipa kodi ya eneo langu hapa, mtaji wangu na kutunza mazingira na kuandaa chakula kwenye hali safi,” amesema Victoria.

Kwa upande wake Paschal John ambaye ni baba lishe mtaa wa Soweto jijini Mbeya, amesema hajawahi kufikiwa na mtaalamu yeyote kumuuliza suala la kupima afya na hajui ni nini wanapima.

“Kwa hiyo tunaenda hospitali, kituo cha Afya au Zahanati? Labda tuwasubiri hao wataalamu waje kutupima watupe maelekezo ili tujue tunafanya nini, binafsi nazingatia usalama wa chakula,” amesema John.

Kwa upande wake mama lishe Jesca Mwashilindi amesema hilo ni suala la kisheria na kuwa kabla ya kufungua biashara hiyo alizingatia utaratibu.

“Kwanza walinipa elimu maofisa afya, huwa wanapita kila eneo na mimi nilipima nikapewa cheti, japokuwa inanipa ugumu wa kupima hawa wasaidizi wangu wanaokuja, kwa kuwa wengi hawakai sana.

Agustino Novat mkazi wa Chimala mkoani Mbeya amesema baadhi ya migahawa haina sifa na wakati mwingine huduma zao zinatia hofu kutokana na kutozingatia sheria na taratibu.

“Muda mwingine unakula chakula sehemu ila tumbo litanguruma, mwisho utavimbiwa na hata hivi vitambi wengine si vya kiafya, ni kutokana na gesi za vyakula tunavyokula mtaani.

“Unakuta mtu kaweka nyama choma barabarani anauza kwa pesa kidogo mzigo mwingi, unajiuliza huyu amepata wapi nyama hizi hadi kuuza hivi, lakini matokeo yake tumbo halitaisha kuuma,” amesema Novat.

Wadau wa afya na mazingira

Titus Shaban ambaye ni mdau wa afya na mazingira amesema chakula ndio msingi wa maisha ya binadamu na kinahitaji uangalizi kuanzia ndani hadi nje na kuwa inapofanyika bila kuzingatia sheria madhara ni makubwa.

“Niwaombe wakati wakitafuta riziki, wazingatie usafi wao kimwili kuanzia kuoga hadi nguo wanazovaa na mahali anapoandalia chakula pawe pasafi, vinginevyo madhara ni makubwa hata kwao.

Picha mbalimbali zikionesha  baba lishe akiendelea na shughuli zake za migahawa katika maeneo tofauti ya Sokoine jijini Mbeya

“Wasilazimishe kipato kwenye uhatari, sheria zipo wazi inapofikia hatua kumbana asiweke malalamiko wala huruma, kila mmoja awe balozi wa mazingira na afya ili tulinde afya zetu,” amesema Shaban.

Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na idara za afya imekuwa ikitoa elimu kwa wauzaji wa chakula kuanzia ngazi ya kata kuhusu usafi na viwango vinavyotakiwa.

Amesema maeneo yote ya biashara yamesajiliwa na biashara katika mazingira machafu au bila kuzingatia sheria, ikiwamo kutovaa sare, hatua zibachukuliwa kwa kushirikiana na serikali za vijiji na halmashauri.

Ofisa Afya Mkoa wa Mbeya, Nimrod Kiporoza, amesema Serikali imejipanga kufanya ukaguzi wa kuwabaini na kuwalasimisha wafanyabiashara wasiozingatia sheria.

Amesema hatua ya kwanza ni kutoa elimu, kisha kuwasajili, huku watakaokaidi wakichukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kufikishwa mahakamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *