Dar es Salaam. Hatua ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo kusaini tamko la maridhiano ya kisiasa litakalofungua njia ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, imeibua matumaini ya kumaliza mivutano ya kisiasa iliyodumu kwa miongo kadhaa huku wachambuzi wa siasa wakisema mafanikio yake yatategemea utekelezaji wa makubaliano hayo, kuliko uzuri wa tamko lenyewe.

Hatua hiyo imetajwa kama nyenzo muhimu katika kufungua ukurasa mpya wenye matumaini kwa Zanzibar, lakini wanaonya kuwa historia ya kisiasa ya visiwa hivyo itaifanya safari ya utekelezaji wake kuwa kipimo halisi cha mafanikio ya maridhiano hayo kuliko shangwe zilizotawala wakati wa kusainiwa.

Julai 9, 2026, CCM na ACT Wazalendo zilisaini tamko la pamoja lenye vipengele saba mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na viongozi wengine wa Serikali na vyama vya siasa.

Lengo la tamko hilo ni kufungua njia ya kuundwa kwa SUK pamoja na kufanya mageuzi katika maeneo muhimu ikiwamo Katiba ya Zanzibar, mfumo wa uchaguzi, utumishi wa umma, utoaji wa haki na serikali za mitaa.

Wakizungumza na Mwananchi leo Julai 10, 2026, wadau hao wamesema hatua hiyo ni fursa ya kipekee ya kuijengea Zanzibar msingi wa amani ya kudumu, hata hivyo wametahadharisha kuwa historia ya maridhiano yaliyopita inaonyesha kuwa changamoto kubwa imekuwa utekelezaji wa makubaliano badala ya kuyafikia.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Levocatus Swai amesema tamko lililosainiwa linaashiria utashi wa kisiasa kutoka kwa viongozi wa pande zote mbili, jambo ambalo limekuwa likikosekana katika vipindi mbalimbali vya migogoro ya kisiasa visiwani humo.

Amesema kwa mara nyingine Zanzibar imeonyesha kuwa mazungumzo yanaweza kuwa njia bora ya kutatua tofauti za kisiasa kuliko kuendelea na misuguano ambayo imekuwa ikijitokeza hasa wakati wa uchaguzi.

“Makubaliano haya yanaweza kuwa mwanzo wa ukurasa mpya wa siasa za Zanzibar iwapo viongozi watayasimamia kwa uaminifu na kuweka mbele masilahi ya wananchi, badala ya vyama vyao,” amesema Dk Swai.

Dk Swai amesema maeneo yaliyotajwa katika tamko, yakiwamo maboresho ya mfumo wa uchaguzi, utumishi wa umma, utoaji wa haki na serikali za mitaa, ndiyo yamekuwa kiini cha malalamiko ya kisiasa kwa miaka mingi.

Mchambuzi wa masuala ya siasa Albert Olingerilwe amesema kilichofikiwa kinapaswa kupongezwa, lakini wananchi watapima mafanikio yake kwa matokeo yatakayoonekana badala ya ahadi zinazotolewa.

Amesema hatua ya viongozi wa juu wa Serikali na vyama vya siasa kushiriki moja kwa moja katika mchakato huo, inaongeza uwezekano wa makubaliano hayo kutekelezwa kwa sababu yanapata uungwaji mkono wa kisiasa.

“Historia ya Zanzibar inaonyesha kuwa makubaliano yanapokosa dhamira ya kisiasa huishia kwenye makaratasi. Safari hii viongozi wameonyesha utayari, sasa kinachosubiriwa ni utekelezaji,” amesema Olingerilwe.

Mchambuzi huyo amebainisha kuwa utulivu wa kisiasa utakaotokana na maridhiano hayo unaweza pia kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa Zanzibar unaotegemea sekta za utalii, biashara na huduma.

Amesema wawekezaji na washirika wa maendeleo huzingatia mazingira ya kisiasa kabla ya kufanya uamuzi wa kuwekeza, hivyo maridhiano hayo yanaweza kuongeza imani kwa wadau wa maendeleo.

“Hata hivyo, mafanikio ya mchakato huu yatategemea pia namna wananchi, asasi za kiraia na vyama vingine watakavyoshirikishwa ili kujenga umiliki wa pamoja wa mabadiliko hayo,” amesema.

Kwa upande wake, mwanasheria wa masuala ya Katiba, Antony Makaranga amesema kipengele kinachohusu kupitia mfumo wa uchaguzi na sheria zinazogusa utawala wa sheria, kinaweza kuwa msingi wa kujenga demokrasia imara Zanzibar.

Amesema bila kufanya mageuzi ya taasisi na sheria, hata Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaweza kushindwa kuondoa sababu za msingi zinazozalisha migogoro ya kisiasa.

“Haki, uwazi na usawa katika taasisi za umma ndiyo msingi wa maridhiano ya kudumu. Bila hayo, tofauti zinaweza kujirudia,” amesema Makaranga.

Chadema kutoa tamko

Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Chadema John amesema wamefuatilia suala hilo na wakati mwafaka chama hicho kitatoa tamko.

“Mazungumzo ni nyenzo ya kushugulikia tatizo, sisi Chadema tunaamini, lakini sisi tumesema tunataka mazungumzo yatakayokuwa na wasuluhishi wa kimataifa. Zanzibar kuna wasuluhishi na wapatanishi, mazungumzo ya Zanzibar msingi wake ulijengwa miaka mingi tangu 1999 na jumuiya za kimataifa.

“Zanzibar ni sahihi kuleta wasuluhishi wa kimataifa huku bara si sahihi, tutazungumza wakati ukifika na tutoa mwelekeo. ACT Wazalendo imesaliti harakati za mabadiliko,” amedai Mnyika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *